KAPUMZIKE KWA AMANI TATA MADIBA



Na. M. M. Mwanakijiji .

Mpigania haki za weusi na alama kuu ya udhalimu wa mfumo wa Ubaguzi wa Rangi nchini Afrika ya Kusini Mzee Nelson ‘Madiba’ Mandela amefariki dunia baada yakuugua kwa muda mrefu kufuatia maambukizi ya mapafu kushindwa kutengemaa kwa muda sasa. Mzee Mandela ambaye kwa miezi kadhaa sasa amekuwa akisumbuliwa na matatizo ya maambukizi kwenye mapafu yake amefariki dunia nyumbani kwake ambako alipelekewa toka hospitali ya Moyo ya Mediclinic mjini Pretoria, chini Afrika ya Kusini baada ya familia yake kuomba kufanya hivyo. 

Mzee Mandela alipelekwa hospitali hiyo Jumamosi ya tarehe 8 Juni ikiwa ni baada ya kuanza tena kusumbuliwa na mapafu; miaka ya themanini akiwa kifungoni Mandela alipata ugonjwa wa Kifua Kifuu (TB) kutokana na kazi ngumu ya kupasua mawe kama sehemu ya adhabu ya kifungo chake. Aliondoka hospitali hapo Septemba 1, 2012 baada ya familia kuomba hivyo na kuahidiwa huduma nzuri ya kitabibu nyumbani. Wakati anaondoka hospitali hali yake bado ilikuwa ya utulivu kidogo lakini isiyo na mabadiliko makubwa. Mipango ya mazishi ambayo inatarajiwa kuvuta maelfu ya watu na mamia ya viongozi wa kimataifa inatarajiwa kutangazwa punde.


Mandela akiwa na Walter Sisulu gerezeni Kisiwa cha Robben.

Bw. Mandela (95) alikuwa Rais wa kwanza mweusi wa Afrika ya Kusini kufuatia kutokomezwa kwa utawala wa ubaguzi wa rangi uliofanywa na Makaburu kwa karibu miaka 400 ambapo watu weupe walijipa haki ya kuwatawala na kuwabagua watu weusi. Kabla ya kuwa Rais wa Afrika ya Kusini Mzee Mandela alitumikia kifungo cha miaka 27 jela ambako pamoja na kazi ngumu aliendelea kuongoza kundi la wapigania haki wengine kudai usawa, utu, na umoja wa Waafrika ya Kusini. Mandela alikuwa ni mfungwa maarufu zaidi wa kisiasa duniani ambapo harakati za kutaka afunguliwe zilipiganwa na wanaharakati sehemu mbalimbali duniani licha ya upinzani wa Serikali ya Afrika ya Kusini na Baadhi ya Nchi za Kimagharibi ambazo zilimuona Mandela kama Ghaidi na mchochezi.

Maisha yake ya awali.

Mzee Mandela alizaliwa Julai 18, 1918 katika kijiji cha Mvezo mji mdogo wa Umtatu Jimbo la Cape. Akiwa ni mmoja wa watoto wa Mzee Gadla Henry Mphakanyiswa Nelson Mandela alikulia kwa mamake – mke wa tatu wa Mzee Gadla – katika kijiji cha Qunu ambako pamoja na shughuli nyingine za nyumbani alikuwa mvulana mchunga ng’ombe. 


Baadaye alianza masomo ya shule ya msingi na baadaye Sekondari ambapo aliamini kuwa alikuwa anaandaliwa kwa ajili ya utumishi katika nyumba ya Chifu wa Kabila lake la Xhosa kama mshauri. Hata hivyo baada ya kurudi nyumbani kutoka masomoni mwaka 1940 alikuta kuwa Chifu Jongintaba ameandaa ndoa Nelson Mandela pamoja mtoto wa kiume wa Chifu huyo aitwaye Justice walitoroka nyumbani na kwenda kwenye Jiji la Johannesburg. Alifanya kazi kama mlinzi katika Kampuni ya Madini ya Crown lakini alifukuzwa kazi na msimamizi wa pale baada ya kugunduliwa kuwa alikuwa ametoroka kwao. 


Mandela akiwa amevaa mavazi ya kabila lake la Xhosa; alitoka katika familia ya kichifu.
Kuingia Katika Siasa.

Alipokuwa akiishi kwa muda na mmoja wa binamu zake Nelson Mandela alitambulishwa kwa mwanaharakati wa chama cha ANC Bw. Walter Sisulu ambaye baadaye walifungwa pamoja – Sisulu akitumikia miaka 25 jela. Walter Sisulu alimtafutia kazi ya ukarani katika kampuni ya Wanasheria ya Witkin, Sidelsky and Edelman. Akiwa hapo alifanya masomo ya elimu kwa njia ya Posta ambapo alikuwa anatafuta shahada yake ya kwanza. Mwaka 1943 alihitimu masomo yake ya sheria na kuanza kazi kama Mwanasheria badala ya kurudi kijijini kutumika kwa Chifu. 

Akiwa ameanza kazi kama Mwanasheria Mandela aliendelea kuwa chini ya uangalizi wa Walter Sisulu ambaye alikuwa anaendeleza harakati za kudai haki za weusi. Akikutana mara kwa mara na wanaharakati wengine nyumbani kwa Sisulu Mandela alikutana tena na rafiki yake Oliver Tambo. Ilikuwa ni katika mikutano hiyo alikutana na mwanamama Evelyn Mase ambaye walianza uhusiano wa mapenzi na baadaye kufunga ndoa yake ya kwanza Oktoba , 1944. Walijaliwa watoto wawili wa kiume na wa kike; wa kiume Madiba “Thembi” Thembikile alizaliwa Februari 1946 na wa kike Makaziwe alizaliwa mwaka uliofuatia lakini alifariki miezi tisa baadaye baada ya kupata maambukizi ya ugonjwa uti wa mgongo. 



Mandela na mtoto wake wa kwanza wa kiume Themi.

Baada ya uchaguzi wa 1948 ambapo watu weupe peke yao walishirikia vyama vya Herenigle Nacionale Party na Afrikaner Party viliungana na kuunda chama cha National Party ambacho kilikuwa na sera ya wazi ya ubaguzi na kikapisha na kupanua ukali wa sera ya ubaguzi kupitia sheria mbalimbali za ubaguzi wa rangi. Serikali ya Kikaburu ikaja na mojawapo ya Sheria kali kabisa za kupambana na wanaharakati ambayo inajulikana kama Ukandamizaji wa Ukomunisti ya 1950. Sheria hii ilikuwa inashughulikia karibu mambo yote yanayohusiana na kuipinga serikali na ikiwahusu watu wote. 

Migongano kati ya ANC na Serikali ya Kikaburu ilianza kupamba moto.

Mwaka 1952 Nelson Mandela alikamatwa na utawala wa Makaburu kwa kile kilichodaiwa kujihusisha na vitendo vya Kikomunisti chini ya ile sheria iliyopitishwa miaka michache nyume. Alihukumiwa miezi tisa jela na “kazi ngumu” lakini utekelezaji wa hukumu hiyo ulisitishwa kwa miaka miwili. Lakini mwezi Disemba mwaka huo huo Mandela alipigwa marufuku kuzungumza na zaidi ya mtu mmoja kwa miezi sita. Akiwa kiongozi wa ANC hii ilimaanisha kuwa asingeweza kufanya mikutano na wanachama wake. Mwaka 1953 Mandela na rafiki yake Oliver Tambo walifungua kampuni yao ya Wanasheria katika Jiji la Johannesburg na kuifanya kuwa kampuni ya kwanza ya Wanasheria Weusi katika Afrika ya Kusini. Walijishughulisha na malalamiko mbalimbali ya wananchi hasa yanayohusiana na ukatili wa kisiasa. 

Hata hivyo serikali ikitumia sheria nyingine ikalazimisha kufungwa kwa ofisi hiyo iliyokuwa na wateja wengi na kuihamisha sehemu nyingine ambapo ilikuwa ni vigumu kwa wateja kuifikia. Mwaka 1955 Mandela na wenzake walishirikiana kuandaa kongamano kubwa la watu wa Afrika Kusini ambao wanaamini katika taifa moja la watu wamoja japo wanatoka katika makabila na rangi mbalimbali. 

Katika kongamano hili kulisainiwa kile kinachoaminika kama mojawapo ya nyaraka muhimu kabisa za kutetea usawa na utu wa watu wote ambayo ilijulikana kama Freedom Charter. Kufananisha hii ni sawasawa na Azimio la Uhuru la Marekani au ile nyaraka ya Waingereza ya Magna Carta. Kwa Tanzania tunaweza kufananisha kabisa na Azimio la Arusha. Freedom Charter ilitengeneza ramani ya kujenga taifa la watu walio huru na sawa katika Afrika Kusini. 

Nelson Mandela na Oliver Tambo – wanasheria


Marafiki wawili – miaka mingi toka Kisiwa cha Robben
Hata hivyo kwa upande wa familia ndoa yake kwa Evelyn ilianza kuwa matatani. Kulikuwa na tuhuma za kukosa uaminifu ambapo alidaiwa kuwa na mahusiano ya mapenzi na baadhi ya kina dada wa ANC. Evelyn alijaribu watengane lakini pamoja na jitihahada mbalimbali za kupatana Nelson Mandela aliamua kupeana talaka na mke wake wa kwanza mwezi Machi 1958. Walikuwa wamejaliwa mtoto mwingine wa kike. Wakati huo wa mchakato wa talaka Nelson Mandela alikuwa ameanza mahusiano na Winnie Madikizela mmoja wa wafanyakazi wa mambo ya kijamii. Walifunga ndoa Mwezi Juni 1958.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Inaendeshwa na Blogger.

Wanaofuata

TANGAZO

My Blog List