MIRADI MIKUBWA YA BARABARA KATIKA MIKOA YA RUVUMA NA MTWARA KUSAINIWA


 

Waziri wa Ujenzi, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli kesho atakuwa Mgeni Rasmi katika hafla ya utiaji saini mikataba ya ujenzi wa barabara itakayotekelezwa katika mikoa ya Ruvuma na Mtwara.
Miradi hiyo itahusisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kati ya Namtumbo na Tunduru ambayo imegawanywa katika sehemi tatu ambazo ni Namtumbo – Kilimasera (km 68.20), Kilimasera – Matemanga (km 58.70) na Matemanga-Tunduru (km 60.70).
Tayari Benki ya Maendeleo ya Afrika (ADB) ambayo inayofadhili ujenzi huo kwa pamoja na Shirika la Maendeleo la Japan (JICA), imetoa kibali kwa ujenzi wa sehemu mbili za kuanzia Namtumbo hadi Kilimasera na Matemanga hadi Tunduru.  Sehemu kati ya Matemanga na Kilimasera itasubiri kibali kutoka Benki ya Maendeleo ya Afrika ambacho pia kinatarajiwa kutoka hivi karibuni.
Hii ni mara ya pili kwa sehemu hiyo ya barabara kupata makandarasi. Awali kampuni ya Progressive-Higleig Joint Venture kutoka India ndiyo iliyokuwa imeshinda zabuni hiyo mwaka 2010 lakini baadaye ikasimamishwa kutokana na kushindwa kutimiza masharti ya kimkataba na kuonyesha udhaifu katika utekelezaji wa mradi huo.
Katika hatua nyingine kesho pia utasainiwa mkataba wa ujenzi wa sehemu ya barabara inayoanzia Mangaka mkoani Mtwara hadi Nakapanya (km 70.50) katika mkoa wa Ruvuma. Vile vile utasainiwa mradi mwingine wa ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami kuanzia Nakapanya hadi Tunduru (km 66.50) utakaotekelezwa mkoani Ruvuma.
Kusainiwa kwa miradi hii ni faraja kubwa kwa wakazi wa mkoa wa Ruvuma pamoja na mikoa yote ya kusini kwani barabara hiyo ni kichocheo kikubwa kwa shughuli za kiuchumi na kijamii katika maeneo hayo.
Hafla ya utiaji saini wa miradi hiyo itafanyika kesho (Jumatatu) tarehe 17 Februari, 2013 katika Hoteli ya Court Yard (Protea) hapa jijini Dar es Salaam kuanzia saa 3:00 asubuhi.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Inaendeshwa na Blogger.

Wanaofuata

TANGAZO

My Blog List