Rais wa TFF, Jamal Malinzi aliyetangaza mikakati ya kuikwamua Tanzania soka la kimataifa |
Michuano hiyo maalumu itashirikisha mikoa wanachama ya TFF na itakuwa ikichezwa kwa mfumo wa nyumbani na ugenini kwa timu mbili za kanda moja kuchuana na inatarajiwa kutoa wachezaji bora 60 wataoweka kambi ya siku 30 Tukuyu, Rungwe mkoani Mbeya.
Akizungumza na Waandishi wa Habari leo mjini Dar es Salaam, Rais wa TFF Jamal Malinzi amesema michuano hiyo ni maalumu kwa ajili ya kuuunda upya kikosi bora cha Stars, ili kiweze kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika (AFCON) yatakayofanyika mwakani nchini Morocco.
Malinzi alisema jumla ya timu 32 za Tanzania nzima zitashiriki michuano hiyo, kila mechi moja watakuwepo wasaka vipaji watano ‘Scouts’ kwa ajili ya kumulika wachezaji bora, pia mechi zote zitakuwa zikirekodiwa.
Baada ya zoezi la kuibua vipaji kwenye michuano hiyo, wasaka vipaji wote watajifungia (retreat) kwa muda wiki moja mjini Lushoto, Tanga kupitia rekodi zote za mechi na kuchagua wachezaji 60 bora, ambao watapelekwa Tukuyu, Mbeya kwa ajili ya mazoezi makali na wataalamu mbalimbali.
Wachezaji hao 60 watachujwa baada ya mwezi mmoja na kubaki 30, ambao watachanganywa na wachezaji wa sasa wa Taifa Stars na baadaye kupatikana kikosi bora kwa ajili ya mapambano ya kuwania kufuzu kwa AFCON.
Malinzi alisema wachezaji wa sasa wa Stars nao watakwenda kwenye kambi hiyo mkoani Mbeya mara baada ya kumalizika kwa Ligi Kuu ya Vodacom (VPL) mwezi Aprili.
“Tunaamini mfumo huo utasaidia kupata vijana wapya wa kuboresha kikosi cha Stars, hatutachagua majina wala kuangalia umri kwa kuwa hiki ni kipindi cha mpito na ni muda mchache umebakia kuelekea kwenye michuano hiyo,” alisema Malinzi.
Machi 5 mwaka huu Stars itashuka dimbani kuumana na Namibia katika mechi ya kirafiki inayotambuliwa na Shirikisho la Soka la Kimataifa (FIFA).
Rais wa TFF, Jamal Malinzi akikabidhi sehemu ya vifaa vya michezo kwa ajili ya michuano maalum ya kusaka kikosi cha Stars leo (Picha kwa hisani ya Lenzi ya Michezo) |
Wakati huo huo Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) limeanza rasmi mikakati ya kuiwezesha timu ya taifa ya Tanzania ‘Taifa Stars’ kufuzu kwa Fainali za mataifa ya Afrika (AFCON) mwakani baada ya kupanga mpango wa timu hiyo kuweka kambi nchini Uholanzi.
Kambi hiyo itakuwa ni maalumu kwa timu hiyo kuweza kujiandaa na hatua ya kufuzu kwa fainali hizo zitakazofanyika mwakani nchini Morocco na kushirikisha jumla ya mataifa 16 yatakayofuzu.
Malinzi alisema wameamua kufanya hivyo ili kurudia historia ya mwaka 1980 ya Stars kufuzu kwa mara ya mwisho michuano ya AFCON, iliyofanyika nchini Nigeria, ambapo Stars iliweka kambi Uholanzi mwaka 1979 na kufanikiwa kufuzu kwa fainali hizo.
“Tumepokea barua ya Shirikisho la Soka Afrika (CAF) inayotueleza kuwa mechi zetu za mchujo zitaanza kati ya mwezi Mei hadi Agosti kutokana na kiwango chetu kuwa chini ya nchi 21 bora za bara hili, hivyo muda si mrefu tunafikiria kurekebisha benchi lote la ufundi kwa pamoja na kuanza mikakati ya timu hiyo.
“Huenda timu yetu ikaanzia hatua ya mchujo kama CAF walivyotuandikia, ikifanikiwa kufuzu katika hatua ya makundi ttumepanga kuweka kambi nje ya nchi katika nchi ya Uholanzi, na huko timu itapata mafunzo ya kisasa ili kufanya vizuri kwenye hatua ya makundi,” alisema Malinzi.
Katika hatua nyingine alisema kwa sasa wameshazungumza na Balozi wa Uholanzi hapa nchini kwa ajili ya mipango yao hiyo, pia wamewataarifu wadhamini wakuu wa Stars, Kampuni ya Bia Tanzania (TBL) kupitia kinywaji chao cha Kilimanjaro Premier Lager ili kuandaa bajeti ya ziara hiyo.
0 comments:
Chapisha Maoni