VIONJO MWEZI MTUKUFU' Mohammad Ali, bondia aliyhesilimu na kutumia ngumi kufikisha ujumbe wa Uisilamu duniani. “Hii ni kazi tu kama nyasi zinavyoota, ndege wanapaa, mawimbi yanagonga mchanga, na mimi napiga watu”.




Akimchakaza mpinzaniwake.
Alizaliwa kama Cassius Marcellus Clay (mdogo) 17 Januari 1942 huko Kentucky. Baada ya kumpiga Sonny Liston na kutawazwa bingwa wa ngumi za uzito wa juu duniani mwaka 1964, clay alitangaza kukubali mafundisho ya dini iliyokuwa ikijulikana kama Nation of Islam, moja ya makundi potofu linalojinasibisha na Uislamu. Alibadili jina lake na kuwa Muhammad Ali. Alisema: “Muhammad Ali ni jina la mtu huru, likimaanisha kipenzi wa Mwenyezi Mungu, nawaomba watu walitumie hili jina popote watakapotaka kuzungumza namimi au kunizungumzia mimi.” Akaamua kubeba lawama kwa uamuzi wake Marekani nzima sanjari na hilo aligoma kujiunga katika jeshi la Marekani katika vita dhidi ya Vietnam. Muhammad Ali hakuitii serikali ya Marekani na alitengwa na jamii za Marekani. Ni muislam mweusi na mpingaji mwenye bidii ambaye atakumbukwa daima kama shujaa wa kupinga vita baada ya kufungiwa kushiriki katika michezo kwa miaka mitatu na nusu kutokana na kukataa kwake kushiriki katika vita. Akielezea kukataa kwake kusimikwa katika jeshi alisema:
“Kwanini nivae gwanda na kusafiri umbali wa zaidi maili 10,000 kutoka nyumbani kwenda kuangusha mabomu na risasi kwa Wavietnam na wakati kwa wale wanaooitwa Wanegro (weusi wa Marekani) kule Lousville wanatendwa kama mbwa na kunyimwa haki zao za kibinadam? Hapana, sitaweza kwenda kokote kusaidia mauaji na kuchoma nyumba za taifa masikini ili kuendeleza ubabe wa hawa mabwana wa watumwa kwa watu weusi dunia nzima. Leo ndio ile siku wa ouvu kama huu kumalizwa. Nimeonywa kwa kufanya hivi naweza poteza mamilioni ya dola lakini ndio nishasema mara ya kwanza na sasa naweza kurudia kwa mara nyengine; maadui wa ukweli wa watu wapo hapa hapa. Sitaiabisha dini yangu, watu wangu na mimi mwenyewe kwa kutumika kutumikisha wale wanaoililia haki yao, uhuru na usawa…Kama ningeona vita hivyo vitaleta uhuru na usawa wa wenzangu milioni 22 hata kusingehitajika shida ya kunitia katika jeshi ningegombea mwenyewe kuungana nao. Sina cha kupoteza kwa kusimama katika imani yangu. Nikipelekwa jela halafu ndio nini?! Tumeshafungwa jela kwa miaka 400.”
Alhamdulillah!
Kwa kweli alipata tabu baada ya hapo kwani alihukumiwa kwenda jela miaka mitano japokuwa alikaa nje kwa dhamana. Pasipoti yake ikafungiwa na Shirika la Ndondi Duniani (World Boxing Association) likamnyang’anya taji la ubingwa na kumsimamisha kupigana kwa muda… na akaweza kutoshiriki katika mapambano yoyote kwa miaka mitatu na nusu kisa ni kuwa na msimamo wa kufata imani yake tu. Maneno ya Ali kwenye gazeti la Sports Illustrated katika wakati huu wa tabu yalikuwa, “Naachia ubingwa wangu, utajiri wangu na hata mustakabali wangu wa maisha ya siku zangu za usoni. Watu wengi mashuhuri walijaribiwa na mitihani kutokana na imani zao za kidini. Naamini nikifaulu mtihani huu nitatoka upya nikiwa mwenye nguvu na jasiri zaidi.” Kukataa kwake kwenda Vietnam kulizagaa katika kurasa za mbele katika magazeti yote duniani. Na mtetezi wakupinga vita mmoja aitwaye, Daniel Berrrigan alisema:
“Umekuwa msukumo mkubwa kwetu sisi katika harakati zetu za kupinga vita…katika uhamisho wake Ali alisema: “Nategemea kwenda mbali kusaidia kuweka watu huru huko Vietnam na wakati huohuo wenzangu hapa [Wamerika Weusi] wanafanyiwa unyama, inauma kweli. Ni bora niwape habari wote wanaodhani nimepoteza mengi, ukweli ni kuwa nimeingiza vingi zaidi. Nina amani moyoni, na dhamiri iliyowazi. Huwa ninaamka nikiwa na furaha na ninapokiendea kitanda huwa na uso wa bashasha na hata kama wakinifunga, basi nitakwenda gerezani huku nikiwa na furaha pia.”
Katika miaka ya kati  ya 1970, alianza kuisoma Qur’an vizuri na ilipofika mwaka 1975, aliingia kuwa Muislamu wa Kisunni, itikadi sahihi ya kiislamu. Imani yake ya mwanzo kutoka katika mafundisho ya Elijah Muhammad (kama wazungu ni ‘mashetani’ na hakuna pepo wala moto) vyote vikabadilishwa na sasa kweli alijitayarisha kwa ajili ya maisha yake ya akhera. Mwaka 1984, Ali alizungumza hadharani dhidi ya itikadi za kujitenga za Louis Farrakhan, alisema, “Anachofundisha hakiendani kabisa na tunayoamini. Anafundisha njia za kufanya harakati za wakati ule wa kiza, hatutaki kuungana na itikadi hizo hata kidogo.”
Malcolm X alikuwa na mchango mkubwa katika maisha ya huyu bingwa wa uzito wa juu duniani mara tatu katika ndondi. Muhammad Ali aliiambia Young Muslim kuwa Malcolm X alikuwa, “…mzungumzaji mzuri, alikuwa sio muoga. Alinisaidia mimi kuingia katika Uislamu.” Kiufupi Muhammad Ali aliopoa mwongozo na ushauri kutoka Malcolm X ambaye alikuwa akikutana naye mara kwa mara. Kabla ya mechi yake na Liston ambaye alichukuliwa kama mpigananji anayetisha na mwenye nguvu zaidi katika wakati wake,  Malcolm X alimshauri Ali kukumbuka Dawud alivyomshinda jitu kubwa Goliath.
Akiongea na gazeti la Al-Madinah, Jiddah tarehe 15 Julai 1989, alisema:
“Nimepatwa na mambo mazuri mengi katika maisha yangu, lakini hisia zilizonijia siku niliyosimama katika mlima Arafat siku ya Hiija, sema kweli zilikuwa za kipekee. Nilihisi niko katika mazingira yasiyoelezeka, kulikuwa na mahujaji zaidi ya milioni moja na nusu wakimuomba Mwenyezi Mungu awasamehe na kuwabariki. Ilikuwa ni furaha kubwa kuona watu wa rangi zote, mataifa yote, wafalme, viongozi wa nchi, watu wa kawaida kutoka mataifa masikini wote wakiwa ndani ya vazi rahisi jeupe wakimuomba Mwenyezi Mungu bila kujiona wala kudharau  wenzao. Ilikuwa ni zoezi tosha la kuonesha itikadi ya usawa katika Uislamu.”
Mohammad Ali akiwa kwenye ibada ya swala!
Baadhi ya vitu alivyoshinda Ali, ni medali ya dhahabu katika michezo ya Olimpiki ya 1960 huko Rome; mshindi wa Taji la Glavu za Dhahabu la Kentucky mara 6; mshindi wa Taji la Glavu za Dhahabu wa Taifa (National Golden Gloves), 1959-60; na mwaka 1996 alichaguliwa kuwasha mwenge wa mashindano ya Olimpiki huko Atlanta; amechaguliwa kuwa miongoni mwa wanandondi wa kukumbukwa wa kimataifa (International Boxing Hall of Fame) mwaka 1990; ameshinda mataji matatu ya uzito wa juu akimshinda Sonny Liston (1964), George Foreman (1974) na Leon Spinks (1978) na hivyo kuwa mwanandondi wa kulipwa pekee kushinda mataji hayo mara tatu. Meneja wake wakati mwnegine huwa anamuita GOAT- linalomaanisha ‘the Greatest of all time’ (Bingwa wa mara zote tangu mchezo huo uanzishwe); 1999 Ali alichaguliwa kuwa mwanamichezo wa karne na kituo cha habari cha Sports Illustrated  na cha BBC; Ali pia amekuwa balozi, akijaribu kuokoa mateka wa Kimarekani wane huko Lebanon mwaka 1985; alikuwa mzungumzaji wa kikosi cha Marekani huko Rwanda mwaka 1996; akaanzisha Mfuko wa Maendeleo ya Jamii wa Muhammad Ali huko Chicago, Illinois. Tuzo nyengine alizowahi kupokea ni pamoja na Tuzo ya Jim Thorpe (Jim Thorpe Pro Sports Award, Lifetime Achievement) 1992; Tuzo ya the Essence, 1997; Tuzo ya Arthur Ashe kwa Msaada wake kwa Wote, ESPN (Espy), 1997; Tuzo ya msaaada kwa uongozi wa Marekani (Service to America Leadership Achievement), kutoka kwa Baraza la Taifa la Mfuko wa Waaindishi Habari (National Association of Broadcasters Foundation), 2001.
Xxxxxx
Muhammad Ali alinukuliwa akisema: “Naamini Uislamu. Namuamini Allah na napenda amani.” Na pia alishawahi kusema: “Mimi ni Mmarekani. Ni sehemu msiogundua. Naomba mnizoee. Mweusi, naejiamini, nayejigamba; jina langu sio lenu; dini yangu sio yenu; shabaha zangu sio zenu; mnizoee tu.”
Baadhi ya Dondoo Zake Mashuhuri
“Jogoo anawika akishaona mwanga tu. Muweke katika kiza hatawika. Nimeuona mwanga, nawika sasa.”
□ □ □
“Mtu anayeiona dunia akiwa na miaka 50 sawa na alivyoiona alivyokuwa na miaka 20 atakuwa amepoteza miaka 30 ya maisha yake bure”
□ □ □
“Paa (ogelea) kama kipepeo, choma kama nyuki”
□ □ □
“Yule ambaye hajiamini kufanya jambo lenye hatari, hataweza kushinda chochote katika maisha yake.”
□ □ □
“Chuki zisizo na msingi zipo kwa mtu aliye kizani, akipata mwanga anapona ugonjwa huo”
□ □ □
“Nilichukia dakika zote za mazoezi, lakini nikajiambia, “Usiache, pata tabu sasa, na uishi miaka yako yote iliyobaki ukiwa bingwa.”
□ □ □
“Mimi najulikanaa na kupendwa zaidi, kwani hakukuwa na setilaiti wakati wa Musa na Yesu walivyokuwa duniani, hivyo watu wa mbali hawakuwajua.”
□ □ □
“Kama wanaweza kutengeza Penicillin (dawa) kutoka katika mkate uliooza, bila shaka wanaweza wakatengeneza kitu kizuri kutoka kwako.”
□ □ □
“Siiti majivuno (kujigamba) kama utaweza kuonesha”
□ □ □
“Kunyamaa ni dhahabu kama huwezi kufikiria jibu bora”
□ □ □
“Mtu mwenye uwezo kupita kiasi (superman), hahitaji mkanda wa usalama wa kiti (seatbelt)”
“Ni ngumu kuwa mpole ukiwa na nguvu na ushujaa kama mimi.”
□ □ □
“Kuwa bingwa mkubwa inakupasa uamini wewe ni bora. Kama sio jaribu hata kujidhania.”
□ □ □
“Sijawahi kufikiria kushindwa, lakini leo imetokea, kitu bora ni kufanya lililo sahihi. Hilo ni ombi langu kwa wote wanaoniamini. Wote inabidi tukubali kipigo wakati mwengine maishani”
Alisema hayo baada ya kupigwa kwa mara ya kwanza na Ken Norton 31 Machi 1973.
□ □ □
“Mwenyezi Mungu amenipa ugonjwa huu kunikumbusha mimi sio nambari moja; YEYE ndiye.”
(Kwa sasa Muhammad Ali anasumbuliwa na ugonjwa wa kuetemeka [Parkinson’s disease). Ameanza kusumbuliwa na ugonjwa huo tangia 1984.)
□ □ □
“Siulizi eti kwanini mie? Bila sababu yoyote. Kuna jambo zuri hapo kwani nashkuru nimebarikiwa. Mungu anatujaribu. Mengine mazuri na mengine mabaya. Yote ni mitihani kutoka kwake.”
□ □ □
“Usihesabu siku zifanye siku ndio zihesabu.”
□ □ □
“Mimi ni bora, japokuwa sijapigana bado”
□ □ □
Disemba 2004, mhaojaji wa gazeti la Time, alimuuliza Ali kuhusu ratiba zake ambapo alijibu kwa kusema:
“Nasafiri sana. Nafurahia kukutana na mashabiki wangu. Popote niwapo, swala, kusoma na kutafakari vinachukua nafasi kubwa maishani mwangu. Mimi ni yule yule niliyekuwa mwanzo. Ila nafanya vitu siku hizi kwa upole na taratibu tu. Kuna kitu sijabadilika nacho ni bado hodari.”
Ingawa habari yake inapaswa kutolewa ushahidi, Ali alikwenda kutembelea mabaki ya WTC New York baada ya mashambulizi ya Septemba 11 na aliulizwa na mwanahabari mmoja anajisikiaje kusikia mtu wa dini moja na yake ndio wanaohusika na mashambulizi hayo. Kwa kebehi akamjibi, “Kwani wewe unajisikiaje kila unavyohisi kuwa Hitler naye anashiriki na wewe katika kufata dini ya Kikristo?
Katika mahojiano na Young Muslim akiwepo Lonnie Ali pia, walimuuliza Muhammad Ali: “Nasikia kabla ya kuwa Muislamu, hukuwa msomaji nilifikiri hujui kusoma vizuri” na Lonnie Ali akajibu badala yake akisema:
“Muhammad alikuwa na ugonjwa wa kutoona herufi vizuri (dyslexia) pale alipokuwa mdogo. Na hakutaka kujishughulisha na kusoma lakini sasa anaweza kutumia masaa kadhaa kwa siku akisoma. Wakati anasoma Qur’an ananakili pembeni aya ambayo imemgusa kwa siku hiyo. Anasoma vitabu vya kiislamu, vitabu vya utafiti, hususani vile vinayoongelea mashaka ya Biblia. Huwa anafatilia vizuri kabisa kuangalia kama kuna upendeleo.”
Na kuna wakati Muhammad Ali alionesha hapo kijitabu kinachoitwa Bible Contradictions (Ukinzani/Makosa ya Biblia). Na swali jengine likafata: “Umeshinda ubingwa wa uzito wa juu wa ndondi mara tatu na umefanikiwa kutetea taji hilo mara 19. Zipi ni shabaha zako kwa sasa?” Muhammad Ali akajibu: “Kutangaza Uislamu, hicho tu.” Na akiwa katika mahojiano mengine na mhariri mkuu wa Beliefnet Deborah Caldwell aliyeongea na Hana Ali kuhusu uhusiano wao na baba yake, alisema:
“…baba yangu sasa yupo kiroho zaidi kukilo kidini tu. Ilikuwa muhimu kwake kuwa na dini na kufata mashiko yake aliyoamini miaka ya mwanzo. Kile kilikuwa kipindi tofauti. Sasa anajaribu kuwaita watu katika Uislamu, japokuwa hawezi kama alivyofanya mwanzoni. Afya na mbinu zake za kiroho zimebadilika; sasa hivi anapenda kwenda kuwafanya watu wawe na furaha, kusaidia watu kwa kutoa sadaka…”
YoungMuslim walimuuliza swali, kipi kilikuwa kikubwa kuliko vyote kukipata, nayeye akasema, “Uislamu”. Wakaendelea kumhoji: “Kama ungekuwa na uwezo wa kurudi nyuma na kubadilisha jambo ungefanya nini?” Akasema kwa kujigamba: “Ningekuwa Muislamu nikiwa na miaka 10.” Katika mahojiano hayo walikosea kumuuliza kipi kitabu akipendacho zaidi? Na kama unavyofikiria alivyojibu: “Hilo ni swali la kitoto! Kipi zaidi ya Qur’an.”
Muhammad Ali kwa sasa anaishi Michigan na mke wake wa nne, Yolanda Williams. Muhammad Ali ana watoto tisa: Rasheedah, Jamilah, Maryam, Miya, Khalilah, Hana, Laila, Muhammad mdogo na Asaad. Wakati alipoamua kustaafu mchezo wa ndondi, kauli yake ilikuwa: “Nastaafu kwani kuna mengi mengine mazuri ya kufanya kuliko kupiga watu.”
Kwa kumalizia, tutatoa jibu alilotoa Muhammad kumpa George Plimpton alipomuuliza swali lililomaliza mahojiano yake naye: “Kipi ungependa watu wakikumbuke kwako pale utapokuwa umekwenda?”
“Ningependa waseme, alichukua vikombe kadhaa vya upendo, alichukua kijiko cha uvumilivu, kijiko kimoja cha ukarimu, painti moja ya huruma (galoni moja ina painti 8). Kwati (quart) moja ya tabasamu (kwati sawa na painti mbili), kiasi kidigo cha kujali, na akakoroga niya na furaha, akaongeza imani nyingi, na akachanganya vizuri mchanganyiko wake, na akagawa kwa watu wake wote katika maisha yake, alimhudumia kila mtu aliyestahili alipokutana naye.”
Subhana rabial aalla wabihamdi!
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Inaendeshwa na Blogger.

Wanaofuata

TANGAZO

My Blog List