Waziri wa Habari,Vijana, Utamaduni na Michezo, Dk. Fenella Mukangara akitangaza majina ya wanakamati aliowateuwa kuratibu Mbio za Uhuru mwaka huu nchini. |
Mratibu wa Mbio za Uhuru nchini, Innocent Melleck akizungumza na waandishi wa habari juu ya mipango mbalimbali ya mbio hizo. Kulishoto ni Waziri Dk. Fenella Mukangara. |
Baadhi ya waandishi wa habari wa vyombo mbali mbali nchini wakiwa katika mkutano huo. |
WAZIRI wa Habari, Utamaduni, Vijana na Michezo, Dk. Fenella Mukangara jana alitangaza wajumbe watakaosimamia mbio za Uhuru Marathon ambazo zinatarajiwa kufanyika jijini Dar es Salaam Desemba 8, mwaka huu.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam jana, Dk. Fenella alisema wajumbe wa kamati hiyo itakayokuwa na watu 10 itakuwa na jukumu la kuhakikisha mbio hizo zinafanikiwa kwa kiasi kikubwa.
Kamati hiyo inatarajiwa kuongozwa na Mkuu wa Mkoa wa Dar es Salaam, Said Meck Sadiq huku ikiwa na wajumbe wengine kutoka katika sekta mbalimbali nchini.
Wajumbe wengine katika kamati hiyo iliyoundwa na waziri ni Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Sofia Mjema, Mkurugenzi wa Hifadhi za Taifa (TANAPA), Allan Kijazi, Naibu Mkurugenzi wa Michezo kutoka Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo, Juliana Yassoda na Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Habari, Zamaradi Kawawa.
Wengine ni Mkurugenzi wa Kampuni ya Intellectuals, Innocent Melleck, Kaimu Mhariri Mtendaji wa magazeti ya serikali (TSN), Gabriel Nderumaki, George Kavishe kutoka Kampuni ya Bia Tanzania (TBL), Mhariri Mtendaji wa Uhuru, Jossiah Mfungo na Habib Gunze wa Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania.
Waziri Fenella alisema mbio hizo zitakuwa zimegawanyika katika sehemu nne kukiwa na mbio ndefu za kilomita 42, mbio za kati kilomita 21, mbio za kujifurahisha kilomita 5 na mbio fupi ambazo ni maalumu kwa viongozi zikiwa za kilomita 3.
“Mbio hizi zina lengo kuu la kuimarisha umoja, upendo, mshikamano na amani kwa Taifa letu. Tunategemea Watanzania wengi, ikiwa pamoja na viongozi mbalimbali wa Serikali, dini, wanafunzi wa ngazi mbalimbalio na wananchi kwa ujumla wataungana na kushiriki mbio hizi,” alisema.
Naye Mratibu wa Uhuru Marathon, Innocent Melleck alisema wazo kubwa la kuanzisha mbio hizo ilikuwa ni kutaka kuwakumbusha Watanzania kuuenzi umoja, amani, mshikamano ulipo pamoja na uhuru wetu.
Mratibu huyo alisema, mpaka sasa wanariadha zaidi ya 300 kutoka nje ya Tanzania wameomba kushiriki mbio hizo za aina yake hapa nchini.
“Sisi kama vijana tukaona kuna haja ya kufanya kitu cha kuwakumbusha Watanzania wenzetu kwani tunatakiwa kudumisha urithi wa amani, mshikamano na uhuru wetu tulioachiwa na mababu zetu,” alisema.
Melleck alisema mbali na mbio hizo kufanyika siku hiyo, pia kutakuwa na tamasha kubwa la burudani litakalofanyika katika Viwanja vya Leaders vilivyopo Kinondoni, Dar es Salaam ikiwa ni mkesha wa kusubiri siku ya Uhuru.
Mbali na hayo Waziri Fenella naye alizitaka taasisi mbalimbali kuhakikisha wanazidhamini mbio hizo kwani zina manufaa kiubwa kwa taifa.
0 comments:
Chapisha Maoni