Na Anna Nkinda – Maelezo, Dubai
Mke
wa Rais Mama Salma Kikwete ametunukiwa tuzo ya kimataifa ya Uongozi
wenye Hamasa kwa mwaka 2013 (Global Inspirational Leadership Award 2013)
kutokana na kazi anazozifanya za kuwasaidia wanawake na watoto wa kike
nchini ambazo zimewahamasisha watu mbalimbali Duniani kuweza kuzisaidia
jamii zenye mahitaji.
Hafla
ya kukabidhi tuzo hizo ambazo zilitolewa jana na Kituo cha Maendeleo
ya kiuchumi na Uongozi (CELD) cha nchini Nigeria zilifanyika katika
Hoteli ya Atlantis, The Palm iliyopo Dubai , Umoja wa Falme za Kiarabu
(UAE).
Akiongea
mara baada ya kukabidhiwa tuzo hizo Mama Kikwete ambaye pia ni
Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA) aliwashukuru
waandaaji wa tuzo hizo kwa kuona na kutambua umuhimu wa kazi
anazozifanya na kukipongeza kituo hicho kwa kazi wanayoifanya ya kuinua
uchumi wa wanawake.
Mama Kikwete alisema vifo vingi vya wanawake vinatokana na uzazi, majeraha yanayosababishwa na ukeketwaji, ukatili
wa kijinsia vinaleta wasiwasi na changamoto za kibinadamu hivyo basi
ni lazima wanawake wafanikiwe kukabiliana na hali hii kwa kuwa wengi
wanakufa kutokana na sababu zinazoweza kuzuilika pia wanakosa nafasi ya
kujikwamua kiuchumi.
“Hatuna muda wa kupoteza lazima tuchukuwe hatua sasa bila ya kurudi
nyuma kwa sababu zisizoeleweka nia ni kuweka nafasi yetu ya uongozi wa
kimataifa ambao utakuwa ni mfano wa kujivunia kwa wanawake huku
tukiona kuzaliwa kwa watoto kuwe ni hali ya kufurahia na siyo kipindi
cha huzuni na kuomboleza”, alisema Mama Kikwete.
Alimalizia
kwa kusema tatizo la vifo vya uzazi litaisha pale ambapo juhudi za
makusudi zitafanyika, kuinua hali ya maisha ya wanawake wa Afrika na
nchi zinazoendelea jambo linalotakiwa ni kutambua kuwa Dunia ina
rasilimali za kutosha, utaalamu na ujuzi wa kuweza kufanya mambo hayo.
Kwa
upande wake Mkurugenzi Mtendaji wa Kituo cha CELD Mama Furo Giami
aliwapongeza wanawake hao viongozi kwa tuzo walizopewa na kusema hivi
sasa wanawake wameweza kufanya njia kwa kuthubutu kupita njia ambayo
wanaume walipita hapo zamani na kufanya kazi nzuri zaidi ambayo
imewaletea maendeleo.
Mama
Giami alisema wanawake wengi wenye sauti ndogo wameweza kuzitumia
sauti zao kusikika katika jamii na kukabiliana na changamoto mbalimbali
katika maisha yao. Wameweza kujitegemea na hivyo kupambana na hali
ngumu ya uchumi.
Kituo
hicho ambacho kilitoa tuzo kwa wanawake viongozi 15 kutoka nchi za
Afrika, Asia na Mashariki ya kati kinafanya kazi za kuwainua wanawake na
watoto wanaoishi katika mazingira hatarishi na kuhakikisha kuwa
wanatimiza malengo yao.
Wengine
waliopewa tuzo hiyo ni pamoja na Mke wa Rais wa Namibia Mama Penehufipo
Pohamba, Mke wa Rais wa Burundi Mama Dk. Mchungaji Denise Nkurunziza na
Mke wa waziri Mkuu wa Malaysia Mama Datin Paduka Seri Rosmah Monsor.
Utoaji
wa tuzo hizo ulifanyika mara baada ya kumalizika kwa mkutano wa siku
tatu wa wanawake kutoka nchi za Afrika, Asia na Mashariki ya Kati ambao
ulihudhuriwa na wajumbe kutoka mataifa 28 na kujadili kuhusu Uongozi ni
Elimu: Ufunguo wa mustakabali wa wanawake katika nchi zenye uchumi
unaoibuka.
0 comments:
Chapisha Maoni