UCHAGUZI Mkuu wa Chama cha Waandishi wa Habari za Michezo Tanzania
(TASWA), utafanyika Februari 16 mwaka huu jijini Dar es Salaam.
Uamuzi huo ulifikiwa na kikao cha Kamati ya Utendaji ya
TASWA kilichofanyika Dar es Salaam jana
kujadili masuala mbalimbali ya chama na waandishi wa habari za michezo kwa
ujumla.
Kikao kilikubaliana kuwa uchaguzi ufanyike kwa katiba ya
zamani, kwani mchakato wa katiba mpya unaweza kuchukua muda mrefu, hivyo
kusababisha viongozi waliopo madarakani kuendelea kukalia viti kinyume cha katiba,
jambo ambalo si sahihi.
Kutokana na hali hiyo viongozi wapya watakaochaguliwa moja ya
kazi yao kubwa itakuwa kuifanyia marekebisho makubwa katiba ya chama chetu ili
iende na wakati.
Kikao kimekubaliana kuwa wanachama wote walipie ada zao zote
wanazodaiwa kuanzia mwaka 2011, hadi mwaka 2013, na mwisho wa kufanya hivyo ni
Januari 31 mwaka huu na yule atakayeshindwa kutekeleza agizo hilo atapoteza
haki ya kupiga kura na atahesabika si mwanachama hai.
Malipo yafanywe kwa Mhazini Msaidizi, Mohammed Mkangara,
0658-123082 na hakuna mwanachama mpya atakayekubaliwa kujiunga na chama mpaka baada
ya Uchaguzi Mkuu.
Pia Kamati ya Utendaji imeunda Kamati ya Uchaguzi na kumteua
Mwenyekiti wa zamani wa TASWA, ambaye kwa sasa ni Ofisa Habari wa Shirikisho la
Mpira wa Miguu Tanzania (TFF), Boniface Wambura, kuwa Mwenyekiti wa Kamati ya
Kusimamia Uchaguzi Mkuu wa TASWA, ambapo pia kutakuwa na wajumbe wengine wanne
Wajumbe hao ni Katibu Mkuu wa zamani wa TASWA, Mwina Kaduguda,
aliyepata kuwa Mjumbe wa Kamati ya Utendaji ya TASWA, Peter Mwenda na
wanahabari Isakwisa Mwaifuge na Mbonile Burton ambao wote ni wanachama wa TASWA.
Pia Kamati ya Utendaji imekubaliana tuombe wawakilishi wawili
wawe waangalizi wa uchaguzi huo kuhakikisha haki sio tu inatendeka bali pia
ionekane inatendeka, ambapo mmoja atatoka Baraza la Michezo la Taifa (BMT) na
mwingine Idara ya Habari (MAELEZO), utaratibu wa kuwasiliana na taasisi hizo
mbili unaendelea.
Fomu za kuwania uongozi zitaanza kutolewa Februari 10 hadi
Februari 14 mwaka huu saa kumi alasiri, masuala mengine yahusiyo uchaguzi huo,
ikiwemo mahali utakapofanyika yatatangazwa baada ya kikao cha sekretarieti ya
TASWA na Kamati ya Uchaguzi kitakachofanyika Februari 3.
Si dhambi wanaotaka kuongoza kutangaza nia zao mapema wakiona
inafaa.
Nawasilisha.
Amir Mhando
Katibu Mkuu TASWA
09/01/2014.
0 comments:
Chapisha Maoni