Kanali Mwanakatwe afariki dunia

Aliyekuwa Katibu Mkuu wa Shirikisho la Soka Tanzania (TFF) wakati huo, FAT, Kanali mstaafu Ali Hassan Mwanakatwe amefariki dunia.

Kwa mujibu wa taarifa ya Shirikisho hilo jana kwa vyombo vya habari, Kanali Mwanakatwe alifariki jana asubuhi kwenye Hospitali Kuu ya Jeshi Lugalo jijini Dar es Salaam.

“Kwa mujibu wa binti wa marehemu, Sophia, baba yake alianguka bafuni nyumbani kwake Mbezi Beach ambapo alikimbizwa katika Hospitali ya Lugalo ambapo ndipo umauti ulipomfika wakati madaktari wakimpatia matibabu,” ilieleza taarifa ya Ofisa Habari na Mawasiliano wa TFF, Boniface Wambura.

Kanali Mwanakatwe alichaguliwa kuwa Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Tanzania (FAT) katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1993 mjini Kibaha mkoani Pwani.

Baada ya kuondoka FAT, aligombea nafasi ya Katibu Mkuu wa Chama cha Mpira wa Miguu Mkoa wa Dar es Salaam (DRFA) na kushinda katika uchaguzi uliofanyika mwaka 1997.

“Msiba huo ni mkubwa katika fani ya mpira wa miguu nchini na Afrika kwa ujumla kwani, Kanali Mwanakatwe enzi za uhai wake alitoa mchango mkubwa akiwa kiongozi, na mkufunzi wa utawala wa Shirikisho la Mpira wa Miguu Afrika (CAF). Pia aliwahi kuwa Kamishna wa CAF,” alieleza Wambura.

“TFF tunatoa pole kwa familia ya marehemu Kanali Mwanakatwe, DRFA, na Jeshi la Ulinzi Wananchi wa Tanzania (JWTZ) na kuwataka kuwa na subira na uvumilivu katika kipindi hiki kigumu cha msiba huo mzito.”

Kwa mujibu wa Wambura, taratibu za mazishi zinaendelea kufanywa na familia yake nyumbani kwake Mbezi Beach karibu na Hoteli ya Giraffe wakati ndugu wakisubiriwa kutoka mikoani.

Kifo cha Kanali Mwanakatwe kimetokea siku moja baada ya Tanzania kumpoteza mchezaji wake wa zamani wa Taifa Stars na timu za Simba na Sigara, Gabriel ‘Gebo’ Peter aliyefariki dunia juzi.

Gebo (53), ambaye anatoka katika familia ya soka, ndugu zake ni wanasoka Peter Tino na Emma Peter alitarajiwa kuzikwa jana jioni katika makaburi ya Kigurunyembe mkoani Morogoro.

Aliagwa jana nyumbani kwake Vingunguti jijini Dar es Salaam katika shughuli ambayo ilihudhuriwa pia na Mkurugenzi wa Ufundi wa TFF, Salum Madadi na mtangulizi wake, Sunday Kayuni aliyekuwa kocha wake wakati akiichezea Sigara iliyokuwa na makazi yake Chang’ombe, Temeke.

Kanali mstaafu Ali Hassan Mwanakatwe enzi za uhai wake
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Inaendeshwa na Blogger.

Wanaofuata

TANGAZO

My Blog List