NA SULEIMAN MSUYA
JOPO la Elimu la Waislam (IEP) limesema pamoja na
mafanikio yanayopatikana katika kuhakikisha kuwa elimu ya dini inapatikana
nchini kote bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya uchache wa waalimu wenye
taaluma hiyo.
Hayo yamebainishwa Afisa Mwandamizi wa (IEP) Suleyman
Daud wakati akizungumza na mwandishi wa habari hii jijini Dar es Salaam.
Daud alisema tangu utaratibu huo wa kutoa elimu ya
dini uanze wamepata mafanikio makubwa jambo ambalo linawapatia hamasa ya
kuendelea kuboresha ili uweze kutoa tija kwa vijana wa Kiislaam hapa nchini.
Alisema jitihada zao zimejikita katika kuwapatia
elimu ya dini vijana wakiislam ambao wanamaliza vyuo mbalimbali hapa nchini
kuanzia ngazi ya cheti, stashahada na shahada ili waweze kutoa elimu kwa vijana
wa shule za msingi.
“Napenda kuwaambia Watanzania jamii ya Kiislam kuwa
juhudi zetu zinaenda vizuri za kuwapatia vijana wao elimu ya dini ila
changamoto kubwa ni uchache wa walimu wenye elimu hiyo kuwafundisha” ,alisema.
Afisa Mwandamizi huyo wa (IEP) alisema pamoja na
changamoto hiyo ya uchache wa waalimu mafanikio yamekuwa yakiiongezeka kwa
shule nyingi kuongezeka katika kufanya mitihani hiyo ambayo haina athari yoyote
katika matokeo ya darasa la saba.
Daud alisema katika mtihani wa mwaka jana mikoa 26,
wilaya 94 na shule 2,100 ya Tanzania
Bara na Visiwa zilishiriki watahiniwa walikuwa 68,096 ambapo ufaulu ulikuwa
asilimia 38.04.
Aidha Afisa alisema kwa matokeo ya mwaka huu wa 2014
mtihani ambao ulishirikisha mikoa 26,
wilaya 115, shule 2559 na wahitimu 74192 na ufaulu ni sawa na asilimia 46.45
ambao ni ongezeko la asilimia 8.
Alisema mitihani hiyo itakuwa ikifanyika kila mwaka
kwa wanafunzi wa wakiislam wanaomaliza la saba ambapo lengo lao ni kuhakikisha kuwa ifikapo
mwaka 2017 mitihani hiyo iwe inatambulika kwenye Baraza la Mitihani la Taifa
(NECTA).
Daud alisema pamoja na ukweli kuwa mitihani hiyo
kutotambulika katika baraza la mitihani bado vijana wa kiislaam wamekuwa
wakishiriki bila kuleta pingamizi hasa katika shule ambazo zinaendeshwa kwa
taratibu za kiislaam.
Afisa Mwandamizi huyo alisema katika kufikia malengo
hayo juhudi zinahitajika kutoka kila pande hasa kwa wazazi kwani ni wazi kuwa
elimu hiyo inawajengea uadilifu na upendo vijana hao.
‘Unajua kwa muda mrefu elimu ya dini imekuwa
ikitolewa kwa wanafunzi wa sekondari pekee jambao ambalo imeifanya NECTA
kulitumia somo hilo katika kutafsiri matokeo ya mwanafunzi hivyo lengo letu ni
kuhakikisha elimu hiyo inakuwa rasmi katika elimu ya msingi”, alisema.
0 comments:
Chapisha Maoni