RAIS DKT MAGUFULI AMUAPISHA MKUU WA MAJESHI YA ULINZI, JENERALI MABEYO

Amiri Jeshi Mkuu na Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Jenerali Venance Mabeyo kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi ya Tanzania, Ikulu jijini Dar es Salaam
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli, leo tarehe 06 Februari, 2017 amemuapisha Jenerali Venance Salvatory Mabeyo kuwa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania.
Hafla ya kuapishwa kwa Jenerali Venance Salvatory Mabeyo imefanyika Ikulu Jijini Dar es Salaam na kuhudhuriwa na Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein, Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa, Kaimu Jaji Mkuu Mhe. Prof. Ibrahim Khamis Juma na Mke wa Rais Mama Janeth Magufuli.
Kabla ya kuapishwa kushika wadhifa wa Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania Rais Magufuli amemvalisha Jenerali Venance Salvatory Mabeyo cheo kipya cha Jenerali alichopandishwa kutoka Luteni Jenerali.
Jenerali Venance Salvatory Mabeyo amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Jenerali Davis Mwamunyange ambaye amestaafu.
Aidha, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Luteni Jenerali James Alois Mwakibolwa kuwa Mnadhimu Mkuu wa Jeshi la Ulinzi la Wananchi Tanzania (JWTZ).
Luteni Jenerali James Alois Mwakibolwa amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Jenerali Venance Salvatory Mabeyo ambaye sasa ni Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Tanzania.
Wakati huo huo, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Kamishna Juma Ali Malewa kuwa Kamishna Jenerali wa Magereza.
Kabla ya kuapishwa kushika wadhifa huo, Mhe. Rais Magufuli amevalisha Kamishna Juma Ali Malewa cheo kipya cha Kamishna Jenerali.
Kamishna Jenerali Juma Ali Malewa amechukua nafasi iliyoachwa wazi na Kamishna John Casmir Minja ambaye amestaafu.
Halikadhalika, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Balozi. Luteni Jenerali Mstaafu Paul Meela kuwa Balozi wa Tanzania katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (DRC).
Mhe. Balozi Luteni Jenerali Mstaafu Paul Meela anachukua nafasi ya Mhe. Balozi Antony Ngereza Cheche ambaye amestaafu.
Pia, Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Mhe. Balozi Samuel Shelukindo kuwa Balozi wa Tanzania nchini Ufaransa.
Mhe. Balozi Samuel Shelukindo anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Mhe. Balozi Begum Taj ambaye amestaafu.
Mhe. Rais Magufuli amemuapisha Bw. Nyakimura Mathias Muhoji kuwa Katibu wa Tume ya Utumishi wa Umma.
Bw. Nyakimura Mathias Muhoji anachukua nafasi iliyoachwa wazi na Claudia Mpangala ambaye amestaafu.
Katika hatua nyingine , Mhe. Rais Magufuli ameshuhudia tukio la kuapishwa kwa Mkurugenzi wa Upelelezi wa Makosa ya Jinai Kamishna Robert Boazi Mikomangwa.
Kamishna Robert Boaz Mikomangwa ameapishwa na Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali wa Polisi – Ernest Mangu.
Akizungumza baada ya kuapishwa kwa viongozi hao, Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Majeshi ya Ulinzi Mstaafu Jenerali Davis Mwamunyange kwa kuliongoza jeshi hilo kwa kipindi chote alichokuwa madarakani na kueleza kuwa watanzania wana imani kubwa na JWTZ.
Dkt. Magufuli ametoa wito kwa uongozi mpya wa Jeshi hilo chini ya Jenerali Venance Mabeyo kuendeleza juhudi za kuilinda nchi na pia ametaka majeshi yote hapa nchini yajipange kuendana na sera ya ujenzi wa viwanda kwa kuhakikisha viwanda vya kutengeneza mahitaji yanayoweza kupatikana hapa nchini kwa ajili ya majeshi kama vile sare na vifaa, vinajengwa.
Mhe. Rais Magufuli amempongeza Mkuu wa Jeshi la Polisi nchini Inspekta Jenerali wa Polisi Ernest Mangu kwa kuwasimamisha kazi askari wanaotuhumiwa kujihusisha na biashara ya dawa za kulevya na ametaka juhudi za kupambana na tatizo la dawa za kulevya ziungwe mkono na vyombo vyote vya dola.
Kwa upande wake Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi Mhe. Dkt. Ali Mohamed Shein pamoja na kuwapongeza viongozi wakuu wapya wa JWTZ na kumshukuru Jenerali Mstaafu Davis Mwamunyange kwa utumishi wake amesema Serikali ya Mapinduzi Zanzibar ipo tayari kutoa ushirikiano wowote kwa JWTZ huku akibainisha kuwa ana imani kubwa na Jeshi hilo.

Share on Google Plus

About GLORIA MATOLA

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
Chapisha Maoni

Watch the Video Here

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.

Wanaofuata

Google+ Followers

TANGAZO

My Blog List