HOTEL YA MIKUYU ENEO AMBALO MKUTANO WA TBL ULIFANYIKIA
Kampuni ya Bia Tanzania(TBL) kupitia bia
yake ya Safari Lager imefanikiwa kuwapata washiriki kumi waliofanikiwa kuingia
fainali ya shindano la nyama choma Mkoa wa Mbeya.
Fainali hizo zinatarajiwa kufanyika Machi
2 Jumapili mwaka huu katika viwanja vya Shule ya Msingi Ruanda Nzovwe.
Meneja Matukio wa Kampuni ya Bia Tanzania[TBL]
Kanda ya nyanda za juu kusini, Claud Chawene amesema lengo kuu la mashindano
hayo kuwa ni kuongeza hamasa kwa watayarishaji na walaji wa nyama choma ili kwa
pamoja waweze kufahamu viwango bora katika utayarishaji na uchomaji wa nyama
choma.
Chamwene ameyabainisha hayo alipokuwa
anaongea na vyombo mbalimbali vya habari katika ukumbi wa Hoteli ya Mkuyu
iliyopo Ilomba Jijini Mbeya ambapo awali washiriki walipatiwa mafunzo na
wakufunzi mbali mbali ili kuyafanya mashindano hayo kuwa na ubora.
Amezitaja Baa zilizofanikiwa kuingia
katika mpambano huo unaosubiriwa kwa hamu na wakazi wa Jiji la Mbeya
utakaofanyika katika viwanja vya Ruanda Nzovwe ni pamoja na Baa ya New city
pub,Kalembo,Bonanza Bar,Blue House,Rombo Deluxe na Nebana.
Nyingine ni pamoja na Tarakea Bar,Savoy
Bar,Mbeya City Pub na Iwawa ambapo mshindi wa kwanza atajinyakulia kitita cha
shilingi milioni moja,wa pili shilingi laki nane,wa tatu laki sita,wa nne laki
nne na wa tano atapatiwa shilingi laki mbili.
Aidha Claud amesema mpambano huo
utahanikizwa na muziki wa bendi ya TOT ya Mbeya ambapo mashindano hayo
yanatarajiwa kuwa na msisimko mkubwa kutoka kwa washabiki ambao wamepania
kushuhudia shindano litakaloanza majira ya saa nne asubuhi.
Na Mbeya yetu
|
0 comments:
Chapisha Maoni