Mgeni
rasmi ambaye pia ni Mbunge wa jimbo la Kigamboni Ndugu Faustine
Ndungulile akifungua rasmi Baraza la kazi la UVCCM (W) Temeke mbele ya
Wajumbe (hawapo pichani) lililofanyika kwenye ukumbi wa Malaika uliopo
Kata ya vijibweni, Jimbo la Kigamboni. Picha na Emmanuel J. Shilatu
---------------------------------------
Na Emmanuel J. Shilatu
Mbunge
wa Kigamboni Mhe. Faustine Ndungulile ameanika siri na aina mpya ya
wauzaji wa madawa ya kulevya wanayoitumia katika kupanua wigo wa
watumiaji wa madawa ya kulevya Duniani kupitia watoto wadogo.
Mhe.
Ndungulile aliyasema hayo wakati akifungua Baraza la Vijana la Umoja wa
vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM) kupitia wilaya ya Temeke
uliofanyika katika ukumbi wa Malaika ambapo alibainisha bayana kuwa
wauzaji wa madawa ya kulevya wamekuja na mtindo mpya wa kuwafundisha
watoto wadogo kutumia madawa ya kulevya kupitia kwenye vyakula
wanavyopewa wakiwa mashuleni pamoja na kwenye pipi ambazo watoto hao
wanapozilamba taratibu huanza kujifunza kutumia madawa ya kulevya na
hata katika siku za usoni inawawia vigumu watoto hao kuacha matumizi ya
madawa hayo.
“Wauzaji
wa madawa ya kulevya ni watu hatari sana kwani siku hizi wameanzisha
mtindo wa kuwachanganyia watoto wadogo kwenye vyakula pamoja na kuyapaka
madawa hayo ya kulevya kwenye pipi ambazo watoto hao wanapozilamba
huanza kujifunza matumizi ya madawa ya kulevya tangu wakiwa watoto na ni
ngumu kuchomoka katika mtego wa matumizi ya madawa hayo katika maisha
yao”, alisema Mhe. Ndugulile.
Kama
haitoshi Mhe. Ndungulile alianika bayana matatizo makubwa yanayowasibu
vijana kwa sasa kuwa ni madawa ya kulevya pamoja na maambukizi ya virusi
vya ukimwi ambapo alibainisha waziwazi kuwa nguvu kazi ya taifa la leo
imekuwa rehani kupitia mitego hiyo.
Mbunge
huyo wa Kigamboni ambaye kitaaluma ni Daktari aliweka waziwazi kuwa
licha ya takwimu za kushuka kwa maambukizi ya virusi vya ukimwi kushuka
kutoka asilimia 7 mpaka asilimia 5.1 bado tatizo ni kubwa kupita maelezo
kwa vijana nchini.
“Kati
ya vijana wa kike watatu wanaotumia madawa ya kulevya, wawili kati yao
ambao ni asilimia 67 wameathirika na virusi vya ukimwi. Halikadhalika
kwa upande wa vijana wa kiume wawili wanaotumia madawa ya kulevya,
mmojawao ambaye ni asilimia 50 ana maambukizi ya virusi vya ukimwi. Hali
ni mbaya sana kwa vijana.”Alisema Mhe. Ndungulile.
Mbunge
huyo wa Kigamboni aliwaasa wajumbe hao wa Baraza la UVCCM (W) Temeke na
vijana wote nchini kuwa mbali na matumizi ya madawa ya kulevya na
badala yake wajibiidishe zaidi katika kufanya mambo yenye faida kwao
kupitia shughuli za kiuchumi kwa kuchangamkia fursa zilizopo.
|
0 comments:
Chapisha Maoni