MAMA PINDA: WANAWAKE KUWENI NA NIDHAMU YA MATUMIZI YA FEDHA



IMG_0136MKE WA WAZIRI MKUU, Mama Tunu Pinda amewaasa wanawake nchini kwa kuwataka wawe na nidhamu ya matumizi ya fedha za mikopo wanayochukua kwa ajili kuendeshea miradi kama kweli wanataka kufanikiwa na kutimiza malengo waliyojiwekea.
Ametoa wito huo jana jioni (Jumapili, Machi 9, 2014) wakati akifungua Tamasha la Wanawake (Women Dialogue Front -2014) ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani lililofanyika kwenye hoteli ya JB Belmont, jijini Mwanza. 
Akizungumza na washiriki wa tamasha hilo lililoandaliwa na asasi ya Mikaela Women Empowerment Initiatives  ya jijini Mwanza, Mama Tunu Pinda alisema: “Japokuwa kwenye ujasiriamali kuna changamoto nyingi lakini kuna wenzenu walioweza kufanikiwa. Hivyo nina imani kubwa kuwa nanyi mtafanikiwa, ili mradi muwe na nia ya dhati katika kutekeleza malengo mliyojiwekea.”
Akisisisitiza haja ya kuwa na uthubutu kwenye ujasiriamali, Mama Pinda alisema: “…Lakini niwatake wanawake wenzangu kuwa wajasiri na wenye kuthubutu na kuwa na mipango inayotekelezeka ili muweze kutimiza ndoto zenu.” 
“Sisi wanawake tunapaswa kujitambua na kuzitumia fursa zilizopo ambazo kama tutazizingatia ipasavyo, zitatusaidia kujenga ustawi wa maisha yetu na jamii kwa maana kukua kwa uchumi kwa mwanamke ni kukua kwa uchumi wa familia, kaya na jamii pia.”
Aliwataka akinamama nchini watumie vizuri fursa za mikopo na wawe waaminifu katika kutumia na kurejesha mikopo hiyo. “Tumieni fursa za mikopo kwa kukopa kwa uaminifu, kimkakati na kwa malengo ili kuendeleza miradi yenu na jamii kwa ujumla,” alisisitiza.
Kwa upande wake, Mama Tunu Pinda alisema ana imani kwamba taasisi za fedha zitatoa kipaumbele katika kutoa mikopo yenye riba na masharti nafuu kwa wanawake wajasiriamali ili kuleta maendeleo ya kweli miongoni mwa akinamama.
Akizungumzia kuhusu maambukizi ya virusi vya ukimwi (VVU) katika jiji la Mwanza, Mama Tunu Pinda aliwataka wanawake hao kuwa makini kwa kujikinga na maambukizi mapya ya VVU kwa vile Jiji hilo lina kiwango cha juu cha maambukizi ya ugonjwa huo. 
“Utafiti unaonyesha kwamba Jiji la Mwanza linashika nafasi ya 11 kati ya mikoa 30 ya Tanzania sawa na asilimia 4.2. Na kati ya hao wanawake ndio wanaongoza kuliko wanaume. Hii inasababishwa na wengi wao kukosa uelewa wa kutosha katika masuala ya afya ya UKIMWI pamoja na kukosekana kwa usawa wa kijamii, kiuchumi na unyanyasaji wa wanawake na wasichana walio ndani na nje ya mahusiano,” alisema Mama Pinda.
Alisema takwimu hizo zinaonyesha ni jinsi gani mwanamke anaweza akuchukua tahadhari mapema na ya haraka katika kupambana na ugonjwa huo hatari. “Lakini pia mimi niseme tu, mwanamke una nafasi kubwa sana katika kupambana na ugonjwa huu kwa kuchukua hatua za dhati na za makusudi katika kujikinga wewe na familia yako kama mwanamke unayejitambua,” aliongeza.
Mapema, akisoma risala yao mbele ya mgeni rasmi, Mwenyekiti wa asasi ya Mikaela Women Empowerment Initiatives, Bibi Edith Mudogo alisema asasi hiyo inayojishughulisha na utoaji wa mikopo midogodogo kwa akinamama, ina jumla ya wanachama 102 ambao wanajihusisha na biashara, kilimo na ufugaji.
Alisema wanakabiliwa na changamoto nyingi zikiwemo kunyimwa mikopo na taasisi za kifedha kutokana na masharti yasiyo rafiki yaliyowekwa na taasisi hizo; ukosefu wa fedha unaowanyima fursa ya kuwafikia wanawake waishio vijijini na usumbufu unaopatikana katika kukopa na kurejesha mikopo ingawa ni kwa kiasi kidogo.
IMETOLEWA NA:
OFISI YA WAZIRI MKUU,
S. L. P. 3021,
DAR ES SALAAM.
JUMATATU, MACHI 10, 2014.
Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Inaendeshwa na Blogger.

Wanaofuata

TANGAZO

My Blog List