Wabunge wataka walindwe na polisi

Mbunge wa Muhambwe, Felix Mkosamali (NCCRMageuzi) ameomba Serikali iwape ulinzi wa polisi wabunge, kama inavyofanya kwa viongozi wengine, wakiwemo wakuu wa mikoa na wakuu wa wilaya.

Ili kutekeleza suala hilo, Mkosamali ameiomba Serikali kupeleka haraka muswada bungeni wa kuanzisha ulinzi huo kwa wabunge, hasa wakati huu ambapo baadhi yao wamekuwa wakitishiwa.

Alisema hayo alipouliza swali la nyongeza, kutokana na swali la msingi la Mbunge wa Kasulu Mjini, Moses Machali (NCCR-Mageuzi).

Swali hilo la msingi liliulizwa na Mkosamali kwa niaba ya Machali.

Mkosamali alisema: “Swali alilouliza Machali linatuhusu wabunge wote. Tunapokuwa humu bungeni wabunge tunauliza maswali mengi yakiwemo yanayohusu wala rushwa. Lakini, tunapotoka nje ya Bunge, hatuna ulinzi. Wenzetu Kenya na Uganda kila mbunge anapewa ulinzi.Tanzania inatoa ulinzi kwa viongozi wa juu, Ma- DC, wakuu wa mikoa na mawaziri. Hapa Serikali inajipendelea. Kwanini hakuna ulinzi kwa wabunge?”

Akijibu swali hilo, Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge) William Lukuvi, alisema ni jukumu la Bunge kushauriana na Serikali kuhusu suala hilo.

Alisema suala hilo inabidi lipelekwe kwenye Tume ya Utumishi wa Bunge, ambako makamishna wa Bunge watalijadili na kupeleka maamuzi yao serikalini.

Pia, Lukuvi alisema wakuu wa wilaya na mikoa siyo watu wadogo, bali ni viongozi wanaosimamia sheria kwa mujibu wa masharti yao ya kazi, hivyo hata ulinzi wanaopewa ni kutokana na masharti ya kazi zao.

Katika swali lake, Machali alihoji: “Hivi sasa viongozi mbalimbali, wakiwemo wabunge wamekuwa wakivamiwa mitaani hata majumbani mwao na kupigwa na watu wasiojulikana. Je, Serikali haioni umuhimu wa kuwapatia wabunge na viongozi wengine askari wa kuwalinda dhidi ya watu wabaya”.

Akijibu swali hilo kwa niaba ya Waziri wa Mambo ya Ndani, Naibu Waziri wa Maji, Amos Makalla alisema ulinzi wa wabunge, viongozi wengine na raia, kwa ujumla wao hutegemea mahitaji mahususi, hasa pale linapojitokeza tishio la usalama.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Inaendeshwa na Blogger.

Wanaofuata

TANGAZO

My Blog List