'Wanawake wasilazimishwe kununua kadi za UWT'

WENYEKITI wa Jumuiya ya Wanawake wa Chama Cha Mapinduzi (UWT) Taifa, Sophia Simba amewataka Wenyeviti na Makatibu wa UWT wa Mikoa na Wilaya kutowalazimisha wanawake kutoa Sh 1,500 kwa ajili ya kununua kadi za uanachama.

Simba ambaye pia ni Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto alisema hayo jana mjini hapa wakati akizindua kikao cha Baraza la UWT la Wilaya ya Dodoma Mjini.

Alisema sasa hali ya maisha ni ngumu kwa hiyo hakuna haja ya kulazimisha wanachama kulipa fedha hizo kwani kuna vyama vingine vimekuwa vikitoa kadi bure kwa wanachama.

“Maisha magumu sasa hivi, wapo wanaoipenda CCM lakini hawana hela tusiwatenge, wenzetu wanatoa hizo kadi bure kwa hiyo hakuna haja ya kufukuza wanachama,” alisema.

Alisema CCM haitafuti hela bali inatafuta ushindi hivyo kuna umuhimu wa kulea wanachama bila kujali hali zao za maisha. “ Hatutafuti hela, tunatafuta ushindi, ikiwa kuna wanaojiweza acheni walipe hiyo Sh 1,500 lakini wengine hawana,” alisema.

Alizitaka jumuiya kubuni miradi itakayosaidia wanawake kuinuka kiuchumi na hivyo kuona umuhimu wa kujiunga na jumuiya hiyo.

Akizungumzia uchaguzi wa Serikali za Mitaa wa mwaka huu, aliwataka wanawake kujitokeza kugombea na kupiga kura katika uchaguzi huo. Alisema akili zote zinatakiwa kuelekezwa kwenye uchaguzi wa Serikali za Mitaa na kuwataka wanawake kujitokeza kugombea kwenye uchaguzi huo na si kubaki kuwa wapiga kura tu.

“Tuunganishe nguvu zetu katika uchaguzi wa Serikali za Mitaa, tuwe kitu kimoja, tuhamasishane kugombea nafasi mbalimbali pamoja na kuwahamasisha wanawake na wanaume wakapige kura,” alisema.

Pia Waziri Simba amewapongeza wakazi wa Morogoro waliotoa taarifa za ukatili aliokuwa akifanyiwa mtoto Nasra Mvungi (4).

Mtoto huyo ambaye kwa sasa ni marehemu alifichwa kwenye boksi na mama yake Mariam Said na kuishi humo kwa muda wa miaka minne bila kupatiwa huduma muhimu kama binadamu.

Alisema kitendo cha majirani wa mtoto huyo kutoa taarifa kwenye vyombo husika kinastahili pongezi pia ni cha kuigwa na kuwataka watu wengine hasa wanawake kutoa taarifa pale wanapohisi au kuona mtoto anafanyiwa ukatili.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Inaendeshwa na Blogger.

Wanaofuata

TANGAZO

My Blog List