*Asema haamini kwamba yeye ni wa hapa hapa
*Yanga wataka ‘Wasauzi’ wajikamue dola 150,000
Ngassa aliposaini Yanga.
NYOTA wa Klabu ya Yanga,Mrisho Khalfani Ngassa aliye kasi uwanjani mithiri ya Mholanzi, Arjen Robben wa Bayern Munich amefunguka na kutoa ya moyoni huku akiusihi uongozi wa Jangwani ulegeze kambanu ili aweze kukipiga katika timu ya Free State Stars ya Afrika Kusini.
Winga huyo mwenye mahaba makubwa na rangi ya njano na kijani, amesema hayo wiki hii nyumbani kwake mtaa wa Tanya, Yombo Dovya saa chache baada ya kurejea kutoka Afrika Kusini alikoenda kujaribu ‘zali’.
Akizungumza na Zunguka Dunia mara baada ya timu yake ya Yanga kumaliza mazoezi kwenye uwanja wa Bandari, Temeke, Ngassa amesema haamini kuwa kipaji chake kinaweza kuishia hapa nyumbani.
Mchezaji huyo anayekipiga pia kwenye kikosi cha Taifa Stars amesema, alipokuwa Afrika Kusini wiki mbili zilizopita, aliivutia timu ya Free State Stars inayocheza Ligi Kuu ya nchini humo, (SABC) ambapo viongozi wake waliahidi kumsajili.
Ngassa anayeaminika kuchota hisia za mashabiki wengi wa Yanga kuliko mchezaji yeyote wa klabu hiyo amesema, huu ni muda mwafaka kwake kucheza nje ya nchi ambapo amedai anaamini kipaji chake kinaweza kunga’aa akiwa na ‘Wasauzi’.
Uongozi wa timu ya Free State ya Afrika Kusini baada ya kuridhishwa na ‘mavitu’ ya Ngassa katika mazoezi aliyofanya, umeweka ofa mezani ukichagiza Yanga ikubali kupokea dola 80,000 ambazo ni sawa na Sh. milioni 130.
Hata hivyo, wakubwa wa Jangwani kupitia kwa Katibu wa Yanga, Beno Njovu wameshaweka wazi msimamo wao kuhusu dau la mchezaji huyo kwamba ili auzwe, ni budi ‘Wasauzi’ wajikamue kwa kutoa kitita cha dola za Kimarekani 150,000 zilizo sawa na Sh.milioni 245 za Tanzania.
Dau hilo linalotakiwa na Yanga, kwa mtazamo wa hali halisi linaonekana kuwa ni mtihani mzito kwa klabu ya Free State ya ‘Bondeni’ ambayo kwa mujibu wa taarifa za uhakika, uchumi wake unadaiwa ni wa kusuasua.
Gazeti hili jana liliwapigia simu Msemaji wa Yanga, Baraka Kizuguto na Katibu wa klabu hiyo, Beno Njovu kutaka watoe ufafanuzi kuhusu kitendawili cha suala la mchezaji huyo.
Kama ilivyo ada, Kizuguto baada ya kuombwa ajibu maswali ya mwandishi wetu, yeye alifura kwa ukali huku akimwelekeza mwandishi ampelekee maswali kwa njia ya maandishi, email.
“Kaka, mabosi wangu wameniagiza kuwa waandishi wanaotaka ufafanuzi wowote kuhusu masuala ya Yanga, waandike maswali yao na kuyatuma kwa njia ya email. Vinginevyo mimi siko tayari kukujibu lolote kuhusu issue ya Ngassa”, Kizugut alikaririwa na Mtandao huu.
Hata hivyo, mwandishi wetu baada ya kukosa ushirikiano na Kizuguto, alimgeukia Katibu mkuu wa Yanga, Beno Njovu ambaye kila alipopigiwa simu yake ya mkononi mara kadhaa haikupokelewa.
Hata hivyo, baadhi ya wana Yanga waliohojiwa kutaka watoe mtazamo wao kuhusu kizungumkuti cha Ngassa, walionyesha kutofautiana.
Wakizungumza na gazeti hili kwa sharti la kutotajwa majina yao, wafuasi hao wa Jangwani wamesema ni vyema uongozi wa Yanga ukamuonea huruma mchezaji huyo ili aende kujaribu bahati yake nchini Afrika Kusini kuliko kumpiga danadana kila mara.
Wamefafanua kuwa, Ngassa amekuwa akigonga mwamba mara kadhaa kucheza soka la kulipwa nje ya nchi kwani aliwahi kugonga mwamba kujiunga na vilabu kadhaa vikiwemo, West Ham United ya Uingereza na El- Mereikh ya Sudan.
“Masikini ‘dogo’ Ngassa. Sijui ana damu ya Kunguni! Maana haiwezekani kila mara awe ni yeye tu, anayekwaa kisiki asiende kucheza nje. Nadhani ipo namna na wala sio bure. Namsikitikia sana mshikaji”, mmoja wa watu waliokutwa katika kijiwe cha Kahawa, kilicho jirani na kituo cha CCM, Yombo Dovya aliieleza Zunguka Dunia.
This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
0 comments:
Chapisha Maoni