^^^^^^^^^^^^^^
Na Anna Nkinda – Maelezo
Watanzania
wametakiwa kutumia maktaba zilizopo kusoma vitabu na machapisho yaliyopo ili
waweze kujiongezea elimu na ufahamu zaidi wa masuala mbalimbali yahusuyo maisha
na elimu kwa upana wake.
Wito
huo umetolewa jana na Mke wa Rais Mama Salma Kikwete wakati akifungua maktaba
ya watoto iliyojengwa na Serikali ya Korea Kusini kupitia Taasisi ya Step
katika shule ya msingi Mzimuni iliyopo wilaya ya Kinondoni jijinii Dar es
Salaam.
Mama
Kikwete ambaye pia ni Mwenyekiti wa Taasisi ya Wanawake na Maendeleo (WAMA)
alisema elimu ni ufunguo wa maisha na kwa njia hiyo Taifa linaweza kupambana na
kushinda vita dhidi ya maadui wakubwa watatu ambao ni ujinga, umaskini na
maradhi na matokeo ya ushindani huo ni kupatikana kwa maendeleo.
“Pamoja
na mafunzo tunayoyapata shuleni, vyuoni na sehemu za kazi bado tunapaswa
kuendelea kusoma zaidi ili kujiweka katika nafasi nzuri ya kupambana na adui ujinga,
maradhi na umaskini”, alisema Mama Kikwete.
Mwenyekiti
huyo wa Wama pia aliwataka walimu wa shule hiyo kutunza maktaba hiyo ili iweze
kukidhi malengo ya kuanzishwa kwake kwa kuandaa taratibu bora za kusimamia
matumizi na kuzuia upotevu na uharibifi wa vitabu na vifaa vingine.
Kuhusu
suala la utandawazi Mama Kikwete alisema ni muhimu jamii
ikatunza na kuimarisha utamaduni ili hali wamo katika utandawazi kwani
hivi sasa Dunia imekuwa kama kiganja cha mkono kutokana na kukua kwa Sayansi ya
Teknolojia ila hayo yote yanawezekana ikiwa watasoma zaidi eneo husika
kulingana na mabadiliko yaliyopo.
Mama
Kikwete alisema, “Leo hii tumepata maendeleo kwa ajili ya Sayansi na Teknolojia
kwani ukitaka kujua chochote kinachoendelea Duniani ni rahisi kwa kuwa unaingia
katika mitandao na kuona, hili ni jambo zuri lakini liendane na mila na
utamaduni wetu siyo kila jambo unalichukua, chukua yale mazuri ambayo
yatakusaidia na yale mabaya ambayo hayana maslahi kwa taifa yaache”.
Kwa
upande wake Balozi Young –Shim Dho ambaye ni Mwanzilishi wa Taasisi ya
Step na Balozi wa mradi wa Utalii endelevu kwa ajili ya kuondoa umaskini wa
Shirika la Umoja wa Mataifa la Utalii Duniani alimshukuru Mama Kikwete kwa
kuifungua maktaba hiyo na kuwataka wanafunzi kuitumia kwa kujisomea.
Balozi
Young –Shim Dho alisema miaka michache iliyopita nchi ya Korea Kusini ilikuwa
ni moja ya nchi maskini Duniani lakini kupitia tabia ya kupenda kusoma
vitabu wamefanikiwa kuwa miongoni mwa nchi zilizomo ndani ya G20 na kuwataka
watanzania kutumia vitabu hivyo kusoma.
“Kujengwa kwa maktaba hii na zingine 23 na kupatikana
kwa vitabu pamoja na vifaa vingine vya maktaba ni jitihada za Mama Kikwete
ambaye alizunguka huku na kule kuomba msaada ambao leo hii umefanikiwa na
kuweza kuwasaidia watanzania wengi”, alisema Balozi Young –Shim Dho.
Ndani
ya eneo la shule ya Msingi Mzimuni kuna shule ya Msingi Mikumi ambapo
Mama Kikwete alimuomba balozi Young –Shim Dho kujenga maktaba kama hiyo kwa
ajili ya shule hiyo na Balozi huyo alikubali na kusema kuwa ifikapo
mwakani maktaba hiyo itakuwa imekamilika.
Hii ni
maktaba ya 24 kujengwa hapa nchini kwa ajili ya watoto wa shule za msingi moja
kati ya hizo ni maktaba ya watu wazima iliyopo ndani ya Jengo la Makumbusho
jijini Dar es Salaam.
0 comments:
Chapisha Maoni