Rage: Kuna mchezo mchafu

Rais wa Klabu ya Simba, Ismail Aden Rage amedai kuwa kuna mchezo mchafu katika usajili wa mlinzi Shomari Kapombe kwenda Azam FC, na kueleza kuwa hawatapokea fedha kiduchu za uhamisho huo.

Inadaiwa Azam FC imemalizana na klabu ya AS Cannes ya Ufaransa kuhusu uhamisho wa mlinzi huyo wa zamani wa Simba ambaye alipelekwa nchini humo, kwa mkataba mahsusi na timu hiyo ya Daraja la Nne.

Kwa mujibu wa Simba, makubaliano yao na AS Cannes ni kwamba endapo Kapombe atauzwa kwa klabu nyingine yoyote, klabu hiyo ya Mtaa wa Msimbazi italipwa asilimia 40 za mauzo hayo.

Lakini taarifa za uongozi wa Simba akiwamo Rage, zinaeleza kuwa Azam FC iko tayari kuwalipa asilimia 40 ya Euro 43,000 (Sh milioni 95.8), wakati taarifa walizonazo wao ni kuwa klabu hiyo ya Chamazi, Temeke, imemnunua Kapombe kwa Euro 107,500, hivyo mgawo na ule wa Cannes unapaswa kuwa Euro 43,000.

Akizungumza na gazeti hili jana, Rage alidai kuwa kuna mchezo mchafu ambao unachezwa na timu ya AS Cannes kuhusu uhamisho huo na kwamba hawatakuwa tayari kupokea fedha ambazo ni kinyume cha mkataba waliosaini wakati mchezaji huyo alipokwenda Ufaransa mwaka jana.

“Hapa kuna mchezo mchafu, kwa nini AS Cannes wakiuke makubaliano wakati kila kitu kiko katika maandishi. Sisi hatutakubali kupokea hizo asilimia 40 ya Euro 43,000 kama ambavyo Azam wametuandikia,” alisema Rage na kuongeza:

“Fedha tunazopaswa kuzipata ni asilimia 40 ya mauzo ya Kapombe. Kwa mujibu wa taarifa tulizonazo, Azam walitaka kumsajili Kapombe kwa Euro 40,000, Cannes wakakataa.

Wakaongeza dau hadi Euro 70,000 bado walikataliwa, na wakatoa Euro 107,500 ambazo wamekubaliwa. Sasa iweje leo watupe asilimia 40 ya Euro 43,000, kwa kigezo gani?

“Hili halitafanyika, na tutashitaki TFF (Shirikisho la Soka Tanzania) hadi FIFA (Shirikisho la Soka la Kimataifa) ili haki itendeke.”

Mwenyekiti wa Kamati ya Usajili ya Simba, Zacharia Hanspoppe alikaririwa jana akiwaonya viongozi wenzake kwamba wasipokee fedha nusu ya Kapombe kwani makubaliano yao ni kulipwa asilimia 40 na As Cannes ya Ufaransa, na si mabingwa hao wa soka Tanzania Bara.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Inaendeshwa na Blogger.

Wanaofuata

TANGAZO

My Blog List