Waziri Wa Elimu na Mafunzo ya Ufundi Dkt. Shukuru Kawambwa amewataka Wakaguzi wa Shule kuhakikisha wanatoa repoti kwa wamiliki wa shule, shule, bodi za shule na kwa walimu baada ya ukaguzi shuleni zinafanyiwa kazi mara moja ili kupunguza changamoto zinazoikabili sekta ya Elimu.
Mhe. Dkt Kawambwa aliyasema hayo hivi karibuni jijini Dar es Salaam katika uzinduzi wa maadhimisho ya Wiki ya Ukaguzi kitaifa iliyofanyika katika ukumbi wa Chuo Kikuu Kishiriki cha Dar es salaam (DUCE)..
“Wamiliki wa shule mnapaswa kufanyia kazi ripoti zinazotolewa na Wakaguzi wa Shule badala ya kuziweka katika makabati, lazima tuhakikishe mapungufu yote yaliyobainishwa yanapatiwa ufumbuzi mara moja ili kuninua ubora wa Elimu.” Alisema Dkt. Kawambwa.
Aidha, amesema ni aibu kwa Wakaguzi wa Shule kuendelea kukagua na kukutana na changamoto zilezile ambazo walikutana nazo wakati walipofanya ukaguzi kwa mara ya kwanza na kuzitolea ripoti kwa wamiliki wa shule na bado hazifanyiwi kazi..
Hata hivyo Dkt. Kawambwa, aliwambia wadau wa Elimu kuwa zipo changamoto nyingi zinazoikabili sekta ya Elimu, ambazo ni pamoja na uhaba wa rasilimali watu, rasilimali fedha, utendaji na usimamizi mbovu, msongamano wa wanafunzi darasani, utoro, uhaba wa walimu wa masomo ya sayansi na hisabati, uhaba wa Majengo, na uhaba wa maabara.
Waziri amesema changamoto nyingi katika sekta ya Elimu zinatokana na ukosefu wa ushirikiano kati ya Wizara na wadau wa Elimu, na hivyo basi kuwaomba wazazi na jamii kwa ujumla kushirikiana kwa pamoja ili kuleta mabadiliko makubwa katika sekta ya Elimu.
Dkt. Kawambwa amewataka wananchi na wadau wa Elimu kuwauliza wakaguzi wa shule, ni mara ngapi wamezikagua shule na wameshauri nini na je ushauri huo umezingatiwa na kufanyiwa kazi, yote hayo yanahitajika ili kufanikisha Mpango mpya wa Matokeo Makubwa Sasa (Bigi Results Now-BRN).
Waziri akiitimisha hotuba yake katika kongamano hilo la wiki ya ukaguzi aliwasihi wadau wa Elimu kuitumia vizuri kauli mbiu ya maadhimisho hayo inayosema “Ukaguzi Fanisi Na Endelevu Kwa Elimu Bora” kujadili kwa kina mada zote katika kongamano hilo zitakazo wasilishwa na wataalamu ili kupata matokeo yanayotarajiwa katika sekta ya Elimu nchini.
0 comments:
Chapisha Maoni