MGM
Grand ilivyotokea kuwa makao makuu ya ndondi - 1
*Floyd Mayweather amepageuza kuwa nyumbani kwake
*Ni hoteli ya pili kwa ukubwa duniani, eneo kubwa USA
LAS
VEGAS, Marekani
FLOYD
Mayweather (zamani Floyd Joy Sinclai ) amepigana mara 12 mfululizo jijini Las
Vegas na kati ya mapigano hayo, 10 ni katika Ukumbi wa MGM Grand Garden Arena.
Alirudiana
hapo wikiendi iliyopita na raia wa Argentina, Marcos Maidana na kumshinda.
"Floyd
anapopigana hapa mambo ni tofauti kabisa. Kuna miale ya umeme usiyoweza
kusimulia. Kuandaa pambano kama hili ni muhimu, si tu kwa hoteli yetu lakini
pia kwa jiji zima. Kuna matukio mengi makubwa, na yote ni muhimu kwetu lakini
pambano la Mayweather linaacha alama yake hapa," anasema Rais wa Michezo
na Matukio wa MGM, Richard Sturm.
MGM
Grand ni hoteli ya pili kwa ukubwa duniani kwa idadi ya vyumba, na kwa maana ya
eneo - migahawa, maeneo ya kupumzikia na kadhalika ndiyo kubwa zaidi kote
nchini Marekani, ikifuatiwa na The Venetian.
MGM
ilipoanzishwa 1993 ilikuwa ndiyo hoteli kubwa zaidi duniani.
Mayweather
ameifanya Las Vegas kuwa nyumbani kwake, binafsi lakini pia katika tasnia ya
ngumi na unaweza kumwona hapa mwaka mzima kwenye jengo kubwa lenye ghorofa 20,
iwe mchana au usiku.
Kila
pambano lake lina thamani ya walau dola milioni 100 kwa uchumi wa Las Vegas
lakini pia kuna mapato mengine ya pauni milioni 11 yasiyohusiana na kamari za
kutabiri bingwa hapa, na mamilioni hayo yanaingizwa kutokana na mapato ya
kwenye migahawa, vyumba vya hoteli na mengineyo.
"Las
Vegas ni Jiji la mwanga, kila kitu ni kizuri, hapa ndipo nilipoanzia tasnia ya
ngumi na hapa ndipo itakapoishia. Ni moja ya sehemu nzuri zaidi nilizopata
kuona duniani," anasema Mayweather.
Lakini
si huyu tu anayependa hapa, wanamasumbwi wengi wamekuwa wakipigana hapa, na
kama mtakumbuka tangu zamani pamekuwa kama kivutio kikubwa cha mabondia chini
ya wadhamini maarufu.
Nyota
wengine waliopigana katika jiji hili ni pamoja na Mohammed Ali, Sugar Ray
Leonard hadi akina Mike Tyson , Oscar De La Hoya na wengine wengi ambao
wamekuwa wakiziba ombwe mara tu linapotokezea, kuhakikisha burudani
zinaendelea, pesa zinachumwa na raha zinapondwa.
Baada
ya kushinda pambano lake la wikiendi iliyopita, Mayweather sasa anafikiria nani
tena amwite hapo MGM.
Mayweather
anayejulikana pia kama Pretty Boy ni Mmarekani mwenye umri wa miaka 37 na
ambaye hadi sasa ana utajiri wa dola milioni 295, alizaliwa Grand Rapids,
Michigan.
Katika
muda wake wa kucheza ngumi za kulipwa, ameshinda mara sita ubingwa katika
madaraja matano tofauti ya uzani, rekodi ambayo haikupata kuwekwa na bondia
mwingine.
Madaraja
hayo ni Super Featherweight, Lightweight, Junior Welterweight, Welterweight mara
mbili na Super Welterweight. Hadi sasa ameshinda mapambano yake yote 47 ya
ngumi za kulipwa; hajui kupoteza pambano ni nini.
Miongoni
mwa mapambano hayo, 28 amewaponda wapinzani wake kwa Knockout (KO) na kwa kiasi
kikubwa ni mmoja wa wanamichezo wanaolipwa zaidi duniani, kama si kwamba yupo
juu ya wengine.
Licha
ya kutokuwa na wadhamini wengi anaoingia nao mkataba ili kuvaa vifaa vyao au
kuwatangazia bidhaa zao, kwa mwaka dili za aina hiyo zinamwingizia dola milioni
80 anapopambana.
New
York ndiyo ilikuwa ikitamba zamani kama makao makuu ya ndondi za ulimwengu,
kwani kwa miongo mingi hapo ndipo redio, baadaye televisheni zilijenga mvuto
mkubwa sana kwa watu katika sayansi tamu ya kupigana makonde.
Rekodi
zinaonesha kwamba, ndondi ndio mchezo wa kwanza kabisa kurushwa kwenye
televisheni moja kwa moja na hapo ni wakati Willie Pep alipohifadhi taji lake
kwa kumchapa Chalky Wright mwaka 1944.
Katika
baadhi ya maeneo ndondi zilipigwa karibu kila wikiendi usiku, zikawa maarufu
lakini zikiandamana na machafuko mitaani, vioo vya nyumba za makazi na maduka
vikivunjwa na mashabiki wanazi.
Yanakumbukwa
maeneo kama Garden na Eastern Parkway Arena pamoja na St. Nick's na
Sunnyside Gardens. Kadhalika hatutasahau Gillette na Pabst Blue Ribbon ambamo
mabondia walizichapa na kuna wakati mara tatu kwa wiki pangekuwa na mapigano.
The
Gillette Cavalcade of Sports yalirushwa kutoka Madison Square Garden, na
ilianza rasmi kitaifa kwenye kituo cha televisheni cha NBC mwaka 1946, kabla ya
kuzoeleka, kupendeka na kuwa maarufu kila Ijumaa usiku ukumbini lakini pia
kwenye televisheni. ITAENDELEA WIKI IJAYO.
CHANZO: GAZETI LA SPOTILEO
0 comments:
Chapisha Maoni