Wanafunzi wa Elimu ya Juu wanasubiria Ajira rasmi wamuomba Mh:Rais MAGUFURI KUTOA TAMKO JUU YA AJIRA ZA WATUMISHI WA AFYA NA ELIMU

KIKAO CHA WAZI CHA VIJANA WAHANGA WA AJIRA NA WAANDISHI WA HABARI
DHIDI YA TAMKO RASMI LA RAISI WETU MPENDWA DR. JOHN POMBE MAGUFULI
KUHUSU AJIRA RASMI SERIKALINI.
Ndugu Wandishi wa Habari,
Kwanza kabisa tunamshukuru Mungu  kupata fursa ya kuzungumza  nanyi juu ya suala la tamko Rasmi la Rais wetu mpendwa  juu ya Ajira za serikali.
Pili tunapenda kutoa pole kwa majukumu makubwa ambayo yamekuwa yakimkabili Mheshimiwa Rais wetu kwa maana kuongoza nchi si jambo la kawaida kabisa bali linahitaji umakini na utulivu wa hali ya juu na ndo maana muda mwingine amekuwa akisikika akisema “Ni bora asingekuwa Rais” tunadhani maneno hayo yanatokana na mzigo mkubwa alionao katika kuliongoza taifa letu. Pia tunapenda kumpa shukrani za dhati na pongezi dhidi ya vita ya Rushwa na Ufisadi Tanzania sababu ilikuwa ni kikwazo kikubwa sana kwa vijana na wasomi kupata ajira au hata haki zao za msingi na tunampongeza pia kwa juhudi zake za utekelezaji wa ahadi zake kwa vitendo, mfano kununuliwa kwa ndege ambazo zitatoa fursa nyingi za ajira na kurahisha usafiri na mawasiliano, miundombinu imekuwa kila siku ikiboreshwa kama vile daraja la Kigamboni, Barabara za juu na chini, madaraja makubwa na madogo na kubwa zaidi kufuta karo kwa elimu ya msingi na sekondari.
Ndugu waandishi wa habari, msukumo mkubwa uliotufanya tuombe kukutana nanyi ni kumuomba mheshimiwa RAIS wetu DK. JOHN POMBE MAGUFULI atoe  Tamko Rasmi juu ya Ajira za serikali zinatoka tarehe ngapi, mwezi gani na mwaka gani? Bila ya kuathiri kanuni na taratibu za nchi kwa kuzingatia katiba Sura ya kwanza, ibara ya 18, ibara ndogo ya kwanza(1) na ya pili(2)
Ibara ndogo ya kwanza(1) “Bila ya kuathiri sheria za nchi, kila mtu yuko huru kuwa na maoni yoyote na kutoa nje mawazo yake, na kutafuta, kupokea na kutoa habari na dhana zozote kupitia chombo chochote bila ya kujali mipaka ya nchi na pia ana uhuru wa mawasiliano yake kutoingiliwa kati”
Ibara ndogo ya pili(2) “kila raia anayo haki ya kupewa taarifa wakati wote kuhusu matukio mbalimbali nchini na Duniani kote ambayo ni muhimu kwa maisha na shughuli za wananchi na pia juu ya masuala muhimu kwa jamii”
Ni takribani miezi minne(4) sasa imepita tangu atoe tangazo la kusitisha ajira alilotoa mwezi June 2016, Tamko lake lilieleza kuwa ajira zingeweza kutoka baada ya mwezi mmoja au miwili lakini mpaka sasa tunaona kimya jambo ambalo vijana wengi wanajiuliza maswali ambayo Rais wetu ndiye mwenye kuweza kutujibu.
Sisi vijana tunakumbuka wakati wa kampeni zake katika uchaguzi mkuu wa mwaka jana mheshimiwa Rais aliahidi kumwaga ajira huku akisema nchi yetu ni tajiri sana na yenye rasilimali nyingi.
Baada ya kumchagua tulitegemea kupata ajira kama ahadi zake zilivyokuwa wakati wa kampeni, wengi tuliomaliza 2015 tukitegemea zingetoka Januari lakini haikuwa hivyo, tukategemea februari haikuwa hivyo, tukategemea machi haikuwa hivyo, tukategemea Aprili lakini haikuwa hivyo hadi ilipofika June na yeye mheshimiwa Rais akatoa tamko la kusitisha ajira kwa muda wa miezi isyozidi miwili lakini mpaka sasa imekuwa kiza kwetu sisi vijana tulioko mitaani.
Viongozi mbalimbali wa serikali wakiwemo mawaziri na manaibu waziri wamekuwa wakitoa matamko kwa  nyakati tofauti tofauti kuhusu ajira hizo lakini ahadi ambazo kimsingi hazijatekelezwa kiasi kwamba vijana tumeshindwa kuamini kauli zao hivyo kumsihi Mheshimiwa Rais wetu atuambie kama ajira zipo? Kama zipo tarehe ngapi zitatangazwa? Kwa mfano matarajio yetu yalikuwa tunaajiriwa mwezi wa kwanza au wa pili hivyo tulishindwa
Ni dhahiri kuwa vijana wengi wasio na ajira hasa waliomaliza vyuo vikuu mwaka jana 2015 walikuwa na matarajio makubwa sana ya kupata ajira mapema kabisa ya mwaka huu kutokana na ahadi za Rais wetu kipindi cha kampeni lakini bahati mbaya haikuwa hivyo ambapo mpaka sasa mwaka unakaribia kuisha bila kusikia kauli yoyote yenye matumaini kwetu ili tujue hatima yetu.
Viongozi wengi wa serikali wakiwemo wakuu wa wilaya wamekuwa wakisikika mara kadhaa wakisema vijana wajiari huku wakisahau kuwa hata wao wanaosema hivyo wameajiriwa tena wamekuwa wakibembeleza ili wasipoteze ajira zao, lakini kinachotusikitisha zaidi ni pale viongozi hao hao wanaposhindwa kutambua aina ya mfumo wetu wa Elimu nchini unaowaandaa zaidi vijana kuajiriwa. Viongozi hao wanaposhinikiza vijana kujiajiri je, wamewatengenezea mazingira hayo ya kujiajiri?
Kwa bahati mbaya tupo vijana tuliomaliza vyuo mwaka jana 2015 na wengine mwaka huu 2016 wote tumerundikana mtaani kwa kuwa ule mfumo wetu wa elimu hautekelezeki katika kujiajiri.
Kimsingi sisi vijana tuna morali kubwa kufanya kazi kwa ajili ya maendeleo ya Taifa letu hivyo ndiyo maana tunamuomba mheshimiwa Rais wetu kutoa tamko lake Rasmi kuwa Ajira mwaka huu zipo au hazipo? Na kama zipo ni tarehe ngapi hasa zitatoka?
Wengi wetu tumeshindwa kufanya mambo ya maana tukihofia uwezekano wa  kuharibu mambo yetu tuliyoanzisha kama ajira zikitangazwa. Wengi wetu tumekataa kusaini mikataba na Taasisi binafsi tukihofia kuchukuliwa hatua pale ambapo serikali ingeweza kuajiri na kujikuta mikataba inatubana na wengine wamejikuta wakiacha kazi katika taasisi binafsi kutokana na matamko yanayotolewa na viongozi hata waliotamani kufanya biashara wameogopa kuingiza mtaji wao kwa kuhofia kuharibu miradi pindi tamko litakapotoka mapema. Hakika tumekosa majibu sahihi juu ya tarehe ngapi serikali itatoa ajira, YEYE NDIYE WA PEKEE SASA KUTUJIBU SISI VIJANA LINI SERIKALI ITATOA AJIRA???
Sisi ni wananchi tena vijana wazalendo wa nchi yetu MAMA TANZANIA tunapenda sana kujiajiri lakini hapo pana shughuli ngumu ambayo si ya kawaida kama ambavyo imekuwa ikisikika kwa baadhi ya viongozi tofauti tofauti wa nchi yetu kuwa VIJANA MJIAJIRI.
Mara kwa mara wawakilishi wetu Bungeni  wamekuwa wakiuliza sana juu ya lini serikali itatoa ajira, lakini jambo ambalo limekuwa likitia shaka ni pale ambapo mawaziri wamekuwa wakitoa majibu mepesi na wengine kudanganya umma juu ya lini ajira zitatangazwa. Mfano mzuri ni Naibu waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa(TAMISEMI) mheshimiwa Selemeni Jaffo mwezi wa pili(2) alisema hivi Serikali itaajiri mapema mwezi huu na mwezi wa Nne(4) alisema Serikali ina ajenda kubwa sana ya kuajili walimu wapatao elfu orobaini(40000) na watumishi wa afya elfu kumi mia nane sabini(10870) Lakini mpaka mwezi wa Nne unaisha hakuna utekelezaji wowote uliofanyika, Naibu waziri wa Elimu Mhandisi Stella Manyanya alikiri bungeni kuna ukosefu mkubwa wa walimu mashuleni na serikali itaanza kuajiri mwezi huu (Mei) na Waziri wa Ofisi ya Rais Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (TAMISEMI) Mheshimiwa George Simbachawene alikaririwa akisema akizungumza na vyombo vya habari kuwa ajira zitatoka mara baada ya kupitishwa kwa bajeti ya TAMISEMI. wakati wa Bunge la Bajeti kwa nyakati tofauti baadhi ya Mawaziri/Manaibu waziri akiwemo Mhe Angela Kairuki walikaririwa wakisema ajira zingetoka mara baada ya kupitishwa kwa Bunge la bajeti, swali letu Je, bajeti haijapitishwa? Waziri mkuu wa jamhuri wa Muungano wa Tanzania akiwa katika Ziara alisema Ataajili walimu wengi wa Sayansi mwezi wa saba(Julai) Lakini Mwezi June Mheshimiwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania aliomba kwa kwa masikitiko makubwa kusitisha ajira za watumishi wa Umma kwa mwezi mmoja au miwili,wote tukajiandaa kisaikolojia na kimwili kuwa Tayari kuanza kazi baada ya miezi hiyo miwili kuisha jambo ambalo mpaka sasa halijafanikiwa na hatujapata sababu za kutotangazwa kwa ajira hizo.
Ndugu waandishi wa habari Suala la uhakiki limechukua muda mrefu na halina uwezekano wa kuisha mwaka huu au ujao kwa sababu suala la uhakiki ni endelevu hata sisi Tukiajiriwa bado Tutafanyiwa uhakiki hivyo ni vyema tukaajiriwa ili kupunguza Bajeti ya kuhakiki mara mbili mbili.Tena uhakiki umekuwa kila siku ukija kwa sura Mpya Jambo ambalo limetufanya kuwa na mshangao na kuamua kufanya mkutano huu na nyinyi waandishi.
Ndugu zangu athari za kutokutoa na ajira kwetu sisi vijana  ambao ni dhahiri sasa tumekuwa wengi mno mtaani haiwezi kuonekana muda huu lakini baadae inaweza kuwa kubwa mno. Tumeshuhudia dada zetu wengi waliohitimu mwaka jana wakilazimika kuolewa ndoa ambazo hazipo katika malengo yao huku baadhi vijana wenzetu wakijiingiza katika ukabaji, matumizi ya madawa ya kulevya na  vitendo vingine viovu,Pia kutokana na matamko kuwa mengi ya Viongozi vijana wengi wamejikuta wakilipa madeni kutokana na kuvunja mikataba na kuingia hasara kubwa,Pia ikumbukwe kuwa vijana hao hao ni wadaiwa wakubwa wa BODI YA MIKOPO ambapo tunapaswa kulipa madeni hayo ili wadogo zetu nao wapate mikopo. 
Hivyo tunamuomba mheshimiwa Rais wetu ATOE TAMKO HASA KAMA SERIKALI INAMPANGO WA KUAJIRI? Kama ndio NI TAREHE NGAPI,MWEZI GANI NA MWAKA GANI ITAAJIRI? Tamko hili litampunguzia majukumu mengi aliyonayo na litatoa taswira kwa kila kijana mmoja mmoja kati yetu tunaosubiri ajira. Tamko lako litatusaidia kama ajira hazipo tuanze kupigana na maisha yetu wenyewe na kuacha kusubiri USIKU UTAKAPOKWISHA. Na kama ajira zipo ni bora tufahamishwe muda maalumu wa kutangazwa kwa ajira hizo kwa maana suala la uhakiki ni endelevu haliwezi kuisha hivi leo kwani hata hawa watakaoajiriwa watahakikiwa.
Tupe uhakika wako mheshimiwa Rais ili tuondoe wasiwasi na kama ajira hazipo tuambie pia ili tufanye mambo yetu wenyewe.
Tunatanguliza shukrani, tukipata mwaliko tutakuja kunywa na wewe kahawa Ikulu mheshimiwa Rais.
NI SISI VIJANA WAHANGA WA AJIRA 2015/2016

Share on Google Plus

About GLORIA MATOLA

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
Chapisha Maoni

Watch the Video Here

Loading...
Inaendeshwa na Blogger.

Wanaofuata

Google+ Followers

TANGAZO

My Blog List