Gereji Eneo la wazi
Gloria Matola
16 Oktoba, 2017
Dar es salaam.
Wananchi wa Mtaa wa Msisiri B Manispaa ya Kinondoni Jijini
Dar Es Salaam wameilalamikia Serikali kuruhusu matumizi ya eneo la wazi kujengwa
Gereji isiyokuwa rasmi hali inayohatarisha usalama wa watoto wao kutokana na
kuzagaa kwa vyuma chakavu.
Awali eneo hilo lilitengwa kama eneo la wazi lakini baadae
alikabidhiwa Mfanyabiashara Charles Kombe kwa makubaliano ya kuijengea ofisi
Serikali ya Mtaa na yeye kuruhusiwa kutumia eneo hilo kufyatua matofali ya
saruji.
Matumizi ya awali ya eneo hilo yakabadilika kwa
Mfanyabiashara huyo kufungua Gereji hali iliyowalazimu wananchi hao kupaza
sauti zao.
Kutokana na Malalamiko hayo Star tv ilibisha hodi ofisi ya
Serikali ya Mtaa huo na kukutana na Mwenyekiti aliyethibitisha kumuita
mfanyabiashara huyo mara kadhaa bila mafanikio huku akidai hautambui uongozi
huo.
Star Tv ilifika ofisini kwa mfanyabiashara huyo Charles
Kombe maarufu kama Galilaya kutaka kujua ana lipi la kuzungumza kuhusiana na
malalamiko haya
Galilaya alikiri kuwa alikabidhiwa eneo hilo na uongozi wa
Serikali ya Mtaa ya wakati huo na kukataa kuzungumzia malalamiko hayo kwa kile
alichodai kuna kesi mahakamani kuhusiana na eneo hilo huku akikataa kurekodiwa.
Star Tv ilikwenda mbali zaidi na kumtafuta Mkuu wa Idara
inayosimamia maeneo ya wazi Manispaa ya Kinondoni Dismas Hafidh ambaye naye
alikataa kurekodiwa huku akidai mfanyabiashara huyo kuwa mkorofi.
0 comments:
Chapisha Maoni