Dar es Salaam. Wadau wa elimu nchini wameonyesha kushtushwa na matokeo ya mtihani wa kidato cha sita kuonyesha kuwa asilimia 95.98 ya watahiniwa wamefaulu mtihani huo bila kuwapo na mikakati inayoonekana ya kuboresha kiwango cha ufaulu.
Wakizungumza kwa nyakati tofauti jana, wadau hao walisema pamoja na matokeo hayo kuonyesha ongezeko la ufaulu, wana wasiwasi iwapo matokeo yaliyoandikwa kwenye karatasi yanaakisi ufahamu wa wanafunzi.
Waziri Kivuli wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi, Susan Lyimo (Chadema) alisema hakuna mkakati wowote uliochukuliwa na Serikali kuhakikisha ufaulu unaongezeka, hivyo ni jambo la kushangaza kuona matokeo yanaonyesha wanafunzi wamefanya vizuri kiasi hicho.
“Hapo kinachooneka goli limepanuliwa ili magoli yaingie zaidi kwani kati ya mwaka jana na mwaka huu kitu gani kimefanyika. Ukaguzi wa walimu na wanafunzi haufanyiki, ufaulu unaongezekaje?” alihoji Susan.
Aliongeza kuwa kinachofanyika hivi sasa ni kutaka kuwaridhisha wazazi ambao walikata tamaa kutokana na matokeo mabaya ya wanafunzi wao kwa miaka miwili iliyopita.
“Walimu wanajua kuwa hata wasipofundisha wanafunzi kuna mtu huko juu atawafaulisha tu,” alisema.
Mkurugenzi wa shirika la Uwezo linalojihusisha na masuala ya elimu, Ziada Mgalla alisema wanafunzi waliofaulu wanapaswa kupongezwa iwapo asilimia 95.98 ya ufaulu inawakilisha ufahamu wao.
Alisema historia inaonyesha kuwa wapo baadhi ya wanafunzi ambao walifaulu kwa kiwango kikubwa lakini hawakuwa na uwezo wa kufafanua kile walichokiandika kwenye mitihani jambo linalotia shaka kuwa huenda matokeo ‘yalichezewa’.
“Matokeo hayo hayatakuwa na maana kama wanafunzi waliofaulu hawawezi kuwa na ufahamu unaolingana na matokeo yao. Pia wastani unaozungumzwa lazima mwanafunzi awe amepata kuanzia alama 60 kuendelea kama amepata chini ya hapo hakuna sababu ya kushangilia,” alisema Ziada.
Akizungumzia sababu za shule za umma kufanya vibaya, mkurugenzi huyo alisema kuwa Serikali ijiulize kwa nini walimu wanaofundisha shule hizo wanafunzi wao hufeli, lakini wakienda kufundisha shule za binafsi, wanafunzi wao hufaulu.
“Suala siyo tu kuwa na walimu, wawasikilize wanapolalamika vinginevyo itafika wakati mwanafunzi wa sayansi ataonekana amefaulu lakini akifika kwenye upasuaji akashindwa kufanya kazi taifa likatia aibu,” alisema.
Meneja Utafiti na Uchambuzi wa Sera wa HakiElimu, Boniventura Godfrey alisema wakati watu wanashangilia matokeo hayo yaliyotajwa kuwa ni mazuri yakilinganishwa na miaka iliyotangulia, wadau wa elimu wanapaswa kujiuliza kwa nini shule za umma zilizokuwa zikiongoza miaka ya nyuma zinazidi kufanya vibaya.
Alisema Serikali inatakiwa kuchukua hatua za haraka kukabiliana na tatizo hilo kwa kuwa hata mazingira ya shule hizo kwa sasa yameharibika ikilinganishwa na ilivyokuwa siku za nyuma ingawa zina idadi kubwa ya walimu.
Godfrey alisema matokeo hayo hayana uhusiano wowote na mpango wa Serikali wa Matokeo Makubwa Sasa (BRN) kwa kuwa haiwezekani ndani ya mwaka mmoja kukawa na mafanikio ya kiwango hicho.
“Sijui matokeo haya ni mazuri kwa namna gani kwa sababu wala BRN (Matokeo Makubwa Sasa) haiwezi kuwa na mafanikio ya haraka namna hii.
Ninadhani suala la kuangalia hapa ni kwa nini shule za umma zimefelisha huku za binafsi zikiendelea kuongoza,” alisema
0 comments:
Chapisha Maoni