Tume ya utumishi yajitetea fukuza fukuza ya watumishi

TUME ya Utumishi wa Umma imetaja mamlaka za kinidhamu zinazopaswa kuwachukulia hatua watumishi wa umma wanaobainika kukiuka maadili na sheria za kazi.
Mamlaka zilizotajwa na tume hiyo kuwa na mamlaka hayo ni Rais, Katibu Mkuu Kiongozi, Waziri Mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa, Watendaji Wakuu, Mamlaka za Serikali za Mitaa yaani Baraza la Madiwani na wakuu wa idara au divisheni.
Hivyo tume hiyo imewataka watumishi wa umma waliochukuliwa hatua za kusimamishwa au kufukuzwa kazi na hawakuridhika kupeleka mashauri yao katika tume hiyo ili haki itendeke kwa mujibu wa sheria.
Katibu Msaidizi wa Tume hiyo, Enos Ntuso alisema hayo jana wakati alipozungumzia Sheria ya Utumishi wa Umma Namba 8 ya Mwaka 2002 ambayo inatoa uwezo kwa mamlaka za nidhamu katika utumishi wa umma na kuweka misingi ya namna masuala hayo yatakavyoshughulikiwa.
Alisema kwa mujibu wa sheria hiyo na kanuni zake za mwaka 2003, madaraka ya kuwachukulia hatua za nidhamu watumishi wa umma yapo kwa Rais, kwani ana mamlaka ya kuanzisha au kufuta nafasi za madaraka, kuteua viongozi na watendaji wakuu pamoja na kuchukua hatua za kinidhamu za watumishi serikalini.
Alisema pia Katibu Mkuu Kiongozi ndiye mkuu wa utumishi wa umma aliyepewa uwezo wa kimamlaka katika utumishi wa umma hivyo anaweza kuchukua hatua za kinidhamu kwa mtumishi mwingine yeyote kwa kadri atakavyoona inafaa.
Aliwataja wengine kuwa ni Waziri mwenye dhamana ya Serikali za Mitaa kwa kuwawajibisha wakurugenzi wa mamlaka hizo isipokuwa walioteuliwa na Rais huku watendaji wakuu wakiwa na mamlaka kwa watumishi walio chini yao.
Alisema Baraza la Madiwani ni mamlaka ya nidhamu kwa watumishi walio chini yao katika serikali za mitaa pamoja na wakuu wa idara na divisheni kwa watumishi walio katika masharti ya kawaida.
Alisema ili haki itendeke wakati wa kushughulikia masuala ya nidhamu inatakiwa kwa mujibu wa sheria kabla ya kumchukulia hatua za kinidhamu mtumishi apewe hati ya mashtaka, fursa ya kujitetea na uchunguzi wa awali kufanyika ili kuona kama mtuhumiwa ana tuhuma za kujibu.
Alisema mtumishi anaweza kupumzishwa kazi bila kuathiri maslahi yake kwa siku 90 na akifunguliwa mashtaka ndipo kupumzishwa huko kutakoma na mtumishi anasimamishwa kazi baada ya kupewa hati ya mashtaka baada ya mamlaka ya nidhamu kuridhika.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Inaendeshwa na Blogger.

Wanaofuata

TANGAZO

My Blog List