Wassira mahakamani tena Kupinga Ubunge wa Ester Bulaya

Wafuasi wa Mbunge wa zamani wa jimbo la Bunda Mjini, Steven Wassira, wameendelea kumng’ang’ania mbunge wa jimbo kwa sasa, Ester Bulaya, baada ya kuwaibua hoja sita mahakamani wakiiomba mahakama imng’oe katika kiti hicho huku wakiibua hoja sita za kumng’oa Bulaya katika kiti hicho.

 

Miongoni mwa hoja hizo, ni pamoja na madai ya Bulaya kushindwa kutimiza masharti ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi kwa kushindwa kuwasilisha bajeti ya uchaguzi.

 

Nyingine ni kasoro katika fomu ya matokeo ya kura na Msimamizi wa Uchaguzi kutokumwalifu aliyekuwa Wassira ambaye alikuwa mgombea wa nafasi hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM) kuhudhuria kwenye majumuisho ya kura.

 

Wafuasi hao wa Wassira wanaojitambulisha kama wapiga kura, wamewasilisha sababu hizo katika rufaa yao waliyoikata mahakama ya Rufani, wakiomba mahakama hiyo ibatilishe matokeo yaliyompa ushindi, Bulaya katika uchaguzi mkuu wa mwaka 2015.

 

Wapiga kura hao Massato  Massato, Matwiga Matwiga, Janes Ezekiel na Escetic Malagila,  walikata rufaa hiyo wakipinga hukumu ya Mahakama Kuu Kanda ya Mwanza iliyompa ushindi Bulaya katika kesi ya msingi ya uchaguzi namba 1 ya mwaka 2015, waliyoifungua.

 

Kesi hiyo ilisikilizwa na jopo la Majaji watatu, Mbarouk Mbarouk, Agustine Mwarija na Rehem Mkuye, huku warufani wakikilishwa na mawakili Constantine Mutalemwa na Yassin Membar.

 

Mawakili wa warufani walidai kuwa kulingana na kasoro hizo walizozibainisha uchaguzi huo haukuwa huru na wa haki na kwamba mahakama inapaswa kubatilisha matokeo hayo na kuamuru uchaguzi urudiwe.

 

Akifafanua hoja hizo, Wakili Mutalemwa alisema kuwa katika fomu namba 24B ambayo ni ya matokeo ya ubunge kulikuwa na kasoro ya idadi ya wapiga kura kwani ilionesha kuwa wapiga kura walioandikishwa ni 164794, badala ya 69,369.

 

Wakili Mutalemwa alisema kuwa kwa mujibu wa Msimamizi wa uchaguzi wa jimbo hilo, idadi ya wapiga kura walioandikishwa ndio msingi wa mchakato wa uchaguzi na kwamba kutokana na kasoro hizo, uchaguzi haukuwa huru na wa haki.

 

“Hiyo ni kasoro kubwa inayosimama yenyewe kuweza kuathiri matokeo.”, alisema Wakili Mutalemwa na kuongeza kuwa licha ya kueleza kasoro hiyo, Jaji aliyesikiliza kesi hiyo, Noel Chocha, hakuizingatia na badala yake akasema kuwa haiathiri matokeo.

 

Katika hoja nyingine Wakili Mutalemwa alisema kuwa mjibu rufani wa kwanza, Bulaya hakuwasilisha bajeti ya uchaguzi na kwamba kwa hali hiyo hakutimiza matakwa ya Sheria ya Gharama za Uchaguzi namba 6 ya mwaka 2010.

 

Alisema kuwa kwa mujibu wa kifungu cha 20 (4) cha sheria hiyo, kutokutimisha  sharti hilo ni sababu tosha ya kubatilisha matokeo ya uchaguzi.

 

Pia Wakili Mutalemwa alidai kuwa wakati wa majumuisho ya kura, mgombea wa CCM, (Wassira) wala chama chake hawakuarifiwa wala kualikwa na Msimamizi wa Uchaguzi kuhudhuria majumuisho hayo na kwamba Msimamizi wa Uchaguzi alithibitisha hivyo.

 

Wakijibu hoja hizo, Wakili wa Bulaya, Lissu na Wakili Mkuu wa Serikali, Angela Lushagara na Wakili Mkuu wa Serikali, Obadia Kameya, walisema kuwa warufani hawana hoja za msingi kwa kuwa walishindwa kuitibithia mahakama namna ambavyo waliathirika.

 

Mawakili hao kwa nyakati tofauti walisema kuwa hata kama kulikuwa na makosa katika kujaza idadi ya wapiga kura kwenye fomu ya namba 24B, kasoro hiyo haiwezi kusababisha uchaguzi kuwa batili kwani haikuathiri matokeo, na kwamba si kila kasoro inabatilisha matokeo .

 

Kuhusu hoja ya kutokuwasilisha bajeti ya uchaguzi, Lissu alidai kuwa hilo lilikuwa ni jukumu la warufani, na kwamba mbali na mjibu rufani wa kwanza (Bulaya) kuna watu wengine wanaoweza kuwa na taarifa za mgombea kutokuwasilisha bajeti ya uchaguzi.

 

Aliwataja kuwa ni pamoja na Msajili wa Vyama vya Siasa, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Seriakali (CAG), Makatibu Tawala wa Wilaya na Makatibu Wakuu wa vyama vinavyoshiriki uchaguzi, lakini hao wote hawakuitwa na warufani kuthubitisha madai yao.

 

Pia walipinga hoja ya mgombea wa CCM kutokualikwa kwenye majumuisho ya kura wakidai kuwa alialikwa na kama hakuhudhuria alikuwa na sababu zake tu na kwamba hata hivyo kulikuwapo na mawakala wa chama chake.

 

Baada ya kusikiliza hoja za pande zote, mahakama iliahirishwa shauri hilo, ikisema kuwa inakwenda kuandika hukumu na kwamba pande zote wataarifiwa tarehe ya hukumu hiyo.

Share on Google Plus

About Unknown

This is a short description in the author block about the author. You edit it by entering text in the "Biographical Info" field in the user admin panel.
    Blogger Comment

0 comments:

Inaendeshwa na Blogger.

Wanaofuata

TANGAZO

My Blog List