Mkuu wa Wilaya ya Ilala Sophia Mjema amefungua semina ya mafunzo ya elimu ya mlipa kodi kwa wafanyabiashara raia wa kutoka nchi ya China.
Akizungumza leo Jijini Dar es Salaam DC Mjema amesema lengo la kufanya semina hiyo kwa wafanyabiashara kutoka nchini China ni kuwapa elimu ya masuala mbalimbali ya kodi ili waweze kulipa kwa mujibu wa kanuni na sheria za nchi, kwani Wilaya ya Ilala imekuwa ni kitovu cha biashara huku raia kutoka nchini China wakizidi kuongezeka kila siku.
DC Mjema amefafanua kuwa miongoni mwa mambo ambayo wamelenga kuwaelimisha kiundani ni pamoja na masuala ya uhamiaji, biashara, ajira, ulipaji kodi na ushirikiano baina yao na wafanyabishara wengine, ili adhima ya Rais Magufuli ya kila mmoja kulipa kodi stahiki iweze kutimia kwa maendeleo ya Tanzania na kuboresha mahusiano mazuri na Taifa na China.
Katika hatua nyingine DC Mjema amesema kuwa mahusiano mema na wafanyabiashara wa nchini China litapelekea kwenye Tanzania ya viwanda na watanzania wengi watanufaika kwa kupata ajira kutokana na viwanda vitakavyojengwa, huku akisisitiza wanapoajiriwa watanzania wawekezaji wahakikishe wanawatendea haki wafanyakazi wao na wafanyakazi wanafanyakazi kwa bidii na utiifu kwa kufuata taratibu za nchi hii.
Kwa upande wake Meneja wa Elimu ya Mlipa Kodi kutoka Makao Makuu ya TRA nchini Diana Massala ameeleza kuwa semina hiyo iliyoandaliwa kwa ushirikiano wa DC Mjema, Uhamiaji, Jeshi la Polisi na wao TRA utasaidia katika suala la ulipaji kodi kuendana na biashara zinazofanywa na raia hao kutoka china.
Meneja Massala ameongeza kuwa katika semina hiyo watawasisitizia suala la matumizi ya Mashine za Kieleteoniki (EFD), ili waweze kuchangia kodi kwa maendeleo ya Taifa, ikiwemo ulipaji kodi ya mapato, kodi ya uendelezaji ufundi stadi na wahakikishe wanatoa risiti baada ya kufanya biashara.
Umoja huo wa wafanya biashara wa raia kutoka china umehaidi kuendelea kushirikiana na Serikali katika kila jambo ili kuleta maendeleo Tanzania na kukuza ushirikiano baina ya nchi hizo.
0 comments:
Chapisha Maoni